*JK ateuwa mawaziri na kuwaapisha papo hapo
ALIYEKUWA Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amekimbia aibu ya kutimuliwa katika nafasi yake ya uwaziri baada ya kujiuzulu saa chache kabla ya Rais Jakaya Kikwete kufanya mabadiliko ya baraza lake na mawaziri na kumtupa nje Profesa huyo mtaalamu wa masuala ya miamba.
Jana asubuhi Profesa Muhongo aliwaita waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam na kutangaza kwamba ameamua kuachia madaraka kupisha mvutano wa bunge na Serikali, lakini jioni siku hiyo hiyo Ikulu iliwaita wanahabari na kutangaza mabadiliko ya baraza la mawaziri huku Muhongo akitupiliwa nje nafasi yake.
Akijieleza kwa wanahabari Profesa Muhongo alisema anajiuzulu lakini si kwamba amekula rushwa katika nafasi yake, bali kumaliza mvutano uliopo kati ya Serikali na Bunge baada ya kuibuka kwa sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow ambalo alidai limetawaliwa na mgogoro wa uongozi, siasa, madaraka na chuki binafsi.
Kwa upande wake Rais wa Tanzania, Dk.Jakaya Kikwete katika mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri ameteuwa mawaziri wapya wanane na manaibu waziri watano, huku nafasi zingine ambazo hazija guswa zitabaki kama zilivyo.
Akitangaza Mabadiliko hayo jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu kiongozi Balozi Ombeni Sefue alisema wapya waliongia katika Baraza hilo ni Anne Kilango Malecela na Charles Mwijage.
Alisema George Simbachawene aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameteuliwa kuwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini, huku Eng. Christopher Chiza aliyekuwa Waziri Kilimo, Chakula na Ushirika ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji).
Alisema Dk. Harrison Mwakyembe aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi sasa ameteuliwa kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, huku Mary Nagu aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji) amepewa u-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu).
“…Wiliam Lukuvi aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Uratibu na Bunge) ameteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Stephen Wasira aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, (Mahusiano na Uratibu) ameteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.”
“Samuel Sitta aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ameteuliwa kuwa Waziri wa Uchukuzi. Jenister Mhagama aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Uratibu na Bunge)”
Wengine ni Stephen Maselle aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini ameteuliwa kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), huku Angela Kairuki aliyekuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria ameteuliwa kuwa Naibu Waziri Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Balozi Sefue alisema Ummy Mwalimu aliyekuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria na Anne Kilango Malecela mbunge wa Same Mashariki ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Aidha aliongeza kuwa Charles Mwijage Mbunge wa Muleba Kaskazini ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini.
Hata hivyo mawaziri hao waliapishwa mara baada ya kutangazwa na Rais Jakaya Kikwete ambapo wameapa kuzitumikia nyazifa zao mpya kwa uaminifu na kuilinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano.