WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameridhishwa na maendeleo ya upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dodoma ambapo mpaka sasa ujenzi huo umefikia asilimia 35 ikiwa ni kazi iliyotekelezwa ndani ya siku 18 toka alipotoa agizo hilo mwishoni mwa mwezi juni mwaka huu.
Ametoa kauli hiyo alipokuwa akikagua ujenzi wa uwanja huo na kumhimiza mkandarasi wa Kampuni ya Chico kuendeleza kasi ya ujenzi huo ili kukamilisha kwa wakati uliopangwa na kutoa msisitizo kwa makandarasi wengine wanaotekeleza miradi mbalimbali nchini kujipanga na kufanya kazi kwa ushirikiano ili kukamilisha miradi hiyo kwa muda mfupi kulingana na makubaliano ya mikataba.
“Mradi huu umetupa mfano kama tukijipanga vizuri hata kwenye miradi mingine tunaweza kutekeleza kwa haraka na ubora unaotakiwa, kwa upande wetu kama Serikali tutahakikisha uwanja huu unakamilika haraka ili kuruhusu ndege kubwa kuanza kutua”, amesisitiza Waziri Mbarawa.
Aidha ameongeza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa uwanja huo utakuwa chachu kwa Shirika la Ndege Tanzania ATCL kuwaunganisha watanzania kwa kutoa huduma za usafiri anga katika maeneo mbalimbali nchini na hivyo kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi. Kuhusu suala la kufufua ATCL Waziri Mbarawa amesema kuwa Serikali imeshalipa kiasi cha sh. Bilion 36 sawa na asilimia 40 katika hatua za ununuzi wa ndege mbili.
“Kama ilivyo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano tutahakikisha hatua za ununuzi wa ndege mpya zinafanyika kwa haraka ili kuweza kulifufua shirika letu la ndege na kuweza kuanza kutoa huduma za usafiri wa anga ifikapo mwezi septemba mwaka huu”, amesisitiza Waziri Mbarawa.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa upanuzi wa uwanja huo kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Eng. Mbila Mdemu amesema kuwa mpaka sasa mita 900 imekamilika kwa kuweka tabaka la kwanza lami katika eneo la kuruka na kutua ndege na kazi ya kuchimba na kusawazisha eneo la kurefusha njia imekamilika.
“Kasi ya ujenzi wa uwanja huu unaendelea vizuri kwa kushirikiana na mkandarasi wa kampuni ya Chico na kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati kwa kuzingatia viwango na ubora unaotakiwa”, amesema Eng. Mbila.
Upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dodoma unahusisha njia ya kuruka na kutua kwa ndege yenye urefu wa Km 2.5 na mita 500 za taa za kuongozea ndege na usalama wa kuruka kwa ndege.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.