WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameitaka Mamlaka ya Usafiri wa Nchi kavu na Majini (SUMATRA), kudhibiti wasafirishaji wasio waaminifu, wanaobadilisha ruti za safari na kuongeza nauli nyakati za asubuhi na jioni nchini. Akizungumza na wafanyakazi wa SUMATRA amewataka kutengeneza mkakati utakaoboresha huduma za usafiri na kupunguza ajali za barabarani nchini kote.
“Sumatra mna mchango mkubwa wa kusimamia sekta ya usafirishaji nchini, hatutaki kuona nauli zinabadilika nyakati za asubuhi na jioni na kusababisha usumbufu kwa abiria”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Amewataka SUMATRA kutosita kuchukua sheria kwa yeyote anayekiuka taratibu za usafiri, kujenga mazingira sawia ya ushindani, kusimamia gharama na viwango vya huduma na kutoa leseni kwa wasafirishaji kwa haraka. Waziri Prof. Mbarawa ameipongeza Mamlaka kwa jitihada wanazozifanya za kuweka mifumo ya utendaji wa kieletroniki itakayo ratibu mabasi yawapo safarini ili kupunguza mwendo kasi na kupunguza ajali.
Aidha Waziri Mbarawa ameitaka SUMATRA kukusanya mapato yanayostahili kikamilifu na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima. Kwa upande mwingine Waziri Mbarawa ameitaka Mamlaka hiyo kusimamia mfumo uliopo wa kieletroniki kwa ajili ya kupata leseni kwa muda usiozidi miezi miwili.
Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA Bw. Giliard Ngewe amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa Mamlaka inaendelea kutoa elimu kwa madereva kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kupunguza ajali za barabarani na kuboresha huduma za usafiri nchini.
“Tumejipanga kuhakikisha maeneo yenye upungufu wa mabasi ya abiria yanapatiwa ruti mpya ili kupunguza changamoto katika maeneo ambayo yana changamoto ya usafiri”, amefafanua Waziri Mbarawa Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa ameitaka SUMATRA kuangalia namna ya kutenganisha udhibiti wa usafiri wa majini na Nchi kavu ili kuongeza tija na kukuza sekta hizo hapa nchini.
“Kukiwa na udhibiti wa usafiri wa majini (Maritime Authority) kutasaidia kukuza sekta hiyo na Sumatra kuendelea kudhibiti usafiri wa nchi kavu (reli na barabara)”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa alikuwa katika ziara ya kikazi ya kutoa miongozo na muelekeo wa serikali ya Awamu ya Tano ambapo amesisitiza uadilifu, uwazi, na utendaji kazi wenye malengo yanayopimika, Katika mikakati ya kudhibiti usafiri wa nchi kavu SUMATRA imepanga kuunganisha mikoa yote 25 ya Tanzania Bara kwenye mfumo wa kompyuta ili kutoa leseni kwa haraka na kuongeza mapato ambapo takribani shilingi bilioni 45 zinatarajiwa kukusanywa katika mwaka huu wa fedha.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.