Na Mwandishi Wetu
PROFESA Wamba Dia Wamba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ameunga mkono kauli ya Rais Jakaya Kikwete iliyozua mvutano kati ya Rais wa Rwanda Paul Kagame na Tanzania, na kudai kikwete yuko sahihi.
Profesa Wamba mtaalamu wa historia aliunga mkono kauli ya Rais Kikwete alipokuwa akifanya mazungumzo na baadhi ya wadau wa Mtandao wa Wanabidii waliomtembelea nyumbani kwake nchini Tanzania na kuzungumza naye masuala anuai ya Afrika.
Katika mazungumzo yake Prof. Wamba alisema Rais Kikwete yuko sahihi kwa kauli yake aliyoitoa hivi karibuni mkutanoni akimshauri Rais wa Rwanda kukaa na kuzungumza na makundi anayovutana nayo nchini kwake ya Interahamwe na FDLR ili kumaliza mvutano.
“Mi nadhani Rais Kikwete yupo sahihi kumshauri Rais Kagame kwamba wakae na kufanya mazungumzo ili kumaliza mzozo…na pia kauli hiyo hakuitoa kwa Kagame pekee bali na viongozi wengine wa nchi zikiwemo Uganda, DRC na Rwanda yenyewe, mbona hawa hawakuzua uhasama huo,” alisema Prof. Dia Wamba.
Rais Kagame amekuwa akitoa kauli ya kejeli vitisho kwa Tanzania na Rais Kikwete tangu kutoka kwa kauli ya kumshauri kufanya mazungumzo na makundi wapinzani wake ya Interahamwe na FDLR.
Akizungumzia mgogoro wa DRC Profesa huyo alisema unasababishwa na hila za kimaslahi dhidi ya pande mbalimbali, yakiwemo baadhi ya mataifa ya kimagharibi hasa kwenye madini yanayopatikana eneo hilo.
Akizungumzia mtanzamo wa jumla kwa nchi za Afrika kiongozi huyo alisema anashangaa kuona mambo ambayo awali yalikuwa yakipingwa dhidi ya utawala wa kikoloni yanafanywa sasa na baadhi ya viongozi wa mataifa ya kiafrika tena kwa kiwango kikubwa tofauti na awali ilhali nchi hizo zipo huru.
Aliongeza vitendo vya rushwa, ubinafsi, ubaguzi na matumizi mabaya ya rasilimali za umma bado ni changamoto kwa mataifa mengi ya Afrika na ndiyo vikwazo kwa maendeleo ya wananchi wa nchi hizo.