Prof Mwandosya, Nagu Wataka Katiba Inayotatua Kero za Watanzania

Mbunge Bunge la Katiba, Prof. Mark Mwandosya.

Mbunge Bunge la Katiba, Prof. Mark Mwandosya.


 
Na Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma
 
MJUMBE wa Bunge Maalum la Katiba, Prof. Mark Mwandosya ameeleza kuwa mpaka ifikapo mwaka 2055 Tanzania itakuwa imeachana na umaskini katika nchi ya uchumi wa kwanza endapo kutakuwa na dhamira ya dhati hususani kuwa kuandika Katiba yenye kuleta nafuu kwa watanzania kwani kila kitu kwa Waafrika kinawezekana pasipo kuwa na Wazungu.
 
Prof. Mwandosya alisema hayo jana wakati akichangia mjadala wa katiba ndani ya Bunge Maalum, ambapo alisisitiza umuhimu wa kuwa na katiba itakayozingatia vipaumbele ambavyo vinaweza kumkwamua mwananchi wa kawaida kuondokana na umasikini na kuliinua Taifa kiuchumi. Mwandosya amesema kuwa kuhusu changamoto na kero zinazohusu mambo ya Muungano, katiba imejaribu kuzizingatia karibia zote, huku akieleza kuwa hali ya Muungano ni imara na itaendelea kuwa imara.
 
Ili kufanikisha nchi inapiga hatua baada ya kuwa na Katiba bora, Mwandosya amefafanua kuwa, watumishi wote wa Umma hawana budi kuliletea tija Taifa hili kwa kuwa misingi imewekwa ndani ya rasimu ya katiba na kusisitiza kuwa Mtumishi wa Umma sio mtawala na mambo yanayohusu miiko na maadili ya mtumishi huyo yenye kumtumikia mwananchi serikali Katiba imeweza kuyazungumzia.
 
“Tumezungumzia kuhusu rushwa ambaye ni adui wa haki, kwamba hili tulitambue katika Katiba ili katika Sheria likasimamiwe vilivyo na pia tumezungumzia pia wale wanaouhujumu uchumi,” alisema Mwandosya.
 
Kuhusu haki za vijana, Mwandosya ameeleza kuwa katika Rasimu ya Katiba wamezungumzia juu ya haki za vijana, haki za walemavu, haki za wazee, pamoja na haki za watoto, huku akiwashangaa baadhi ya wajumbe walioko nje ya bunge hilo wanapotoa shutuma kuwa wanapoteza wakati kana kwamba hawazungumzii mambo yanayowahusu wananchi.
 
“Nawaomba wananchi watusikilize na wayazingatie haya tunayoyasema.” Alisema Mwandosya.
 
Akizungumzia kuhusu Vyombo vya Usalama, amesema kuwa Katiba inawalinda na kuwatambua viongozi wa usalama, ambapo sheria inawapa haki hata baada ya kustaafu ili wakaweze kuishi maisha bora kwa kuchukua dhamana kubwa, hivyo kwa dhamana hiyo viongozi hao wanapostaafu wanatakiwa kujiepusha na masuala ya kisiasa kwasababu.
 
“Usalama wa Taifa, Jeshi, Polisi, Magereza na Uhamiaji, hawa tunawatengezea mambo mazuri sana wanapostaafu, kwahiyo tafadhari sana mkishatoka tusaidieni, toeni ushauri lakini mkijiingiza katika siasa na mafaili yetu huku mmeyashika hamtutendei haki,” alisema Mwandosya.
 
Aidha, ameomba kuwepo na Randama kwani hiyo inaandikwa katika lugha ambayo mwananchi anaweza kuisoma tofauti na katiba kwani hiyo inaandikwa kwa lugha ya kisheria, kwahiyo amependekezo kuwepo na randama kwa ajili ya wananchi.
Mwandosya ameongezea juu ya suala la amani kuwa ni jambo kubwa sana, amewananga watu wenye tabia ya kutaka wananchi kuandamana wakapigwe risasi hao ni watu wasioitakia mema nchi, hivyo amewaasa wananchi walipinge kwa nguvu zao zote kuhusu suala hilo.
 
“Nina ushauri kwa viongozi wenye kutaka wananchi wakapigwe risasi na Polisi, naomba watangulie wao wajipige risasi, unapotaka kuwa Shujaa anzia kwanza wewe mwenyewe, usiwapeleke vijana ambao ni matumaini ya nchi yetu, ndugu zangu hili jambo siyo la busara hata kidogo na wananchi mnapokwenda kuandamana, vijana mseme mnaandamana kwa nini? Kwasababu gani? Na kwa misingi gani na kwasababu ya nani? Ukishajibu haya maswali kwakweli mtaona nchi yetu kuwa ni nzuri sana, nchji ya amani”, alisisitiza Mwandosya.

Akichangia mada katika mjadala huo, Mjumbe Mary Nagu alisema Muungano wa Tanzania ni muungano wa damu na wa watu, ambapo Ibara ya kwanza Sura ya kwanza inaeleza kuwa msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano pamoja na katiba iliyopo na inayopendekezwa ni haki ya makubaliaono ya mwaka 1964.
 
Alisema kuwa Hati ya Makubaliano hayo imejengeka katika misingi ya utu, udugu na kuaminiana ambapo Waasisi wa muungano huo hawakupeleka maslahi yao wenyewe binafsi wala kuzingatia suala la mali, bali walizingatia umuhimu na mahitaji ya muungano kutokana na mambo hayo makuu matatu. Ameeleza kuwa mambo wanayoyajadili bungeni hapo kwa sasa ndiyo yatatokana na muungano ambao una mfumo bora na muundo bora.

“Naomba sana tuendelee na kuona kuwa muungano huu ni muhimu nataka niwaambie kwamba Zanzibar ni lango kuu la Jamhuri ya muungano wa Tanzania na lango hili linatuhakikishia usalama wetu na ulinzi wetu kwahivyo na Wazanzibar nao wanufaike na rasilimali za Bara, kwahiyo muungano huu ni muhimu na utanufaisha pande zote mbili mimi sina wasi wasi,” alisema Nagu.
 
Nagu ameleza kuwa usawa wa jinsia utajenga jamii nzuri ya Tanzania ikiwemo kuleta heshima pamoja na haki katika jamii hiyo kwani kwa mila na desturi za Waafrika na Watanzania, wanaume hawakupaswa kuwa wamiliki wa kila kitu.
 
“Akina baba ni Custodians lakini wakajigeuza wamiliki, tunachotaka waendelee kuwa Custodians na sisi watuone ni wenzao, kwa hivyo suala la jinsia halina mjadala, kupitia uwakilishi tuendelee na hamsini kwa hamsini na Katiba iseme wazi, mengine yatajitokeza kwenye Sheria ya uchaguzi.” Alisisitiza Nagu.
 
Kuhusiana na suala la ajira na uongozi Nagu ameeleza kuwa wanawake zaidi ya asilimia 52% wangepaswa kuwa katika kila eneo lakini hawapo na suala hilo linaleta tofauti isipokuwa mashambani ambapo chakula chote kinachotoka kwa kiasi kikubwa wanaolima ni wanawake.