WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewahakikishia wadau wa Maendeleo kuwa Serikali ya Awamu ya Tano iko tayari kupokea changamoto na ushauri utakaoiwezesha kutimiza adhma yake ya kuwa na miundombinu bora na yakisasa itakayoiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya wataalam wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na wadau wa Maendeleo kutoka Benki ya Dunia (WB), Umoja wa Ulaya (EU), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Shirika la Maendeleo la Japani (JICA), Prof. Mbarawa amewahakikishia wadau hao wa maendeleo kuwa wizara yake inatarajia ushirikiano mkubwa hususani katika sekta ya ujenzi wa reli, barabara, bandari na viwanja vya ndege.
“Sekta ya Ujenzi, uchukuzi na mawasiliano inachukua asilimia kubwa ya bajeti ya nchi yetu hivyo licha ya jitihada na misaada mnayotupa bado tupo tayari kupokea misaada, changamoto na ushauri ili ituwezeshe kukamilisha kwa wakati na ubora miradi ya ujenzi inayoendelea na tunayotarajia kuianzisha”, amesema Prof. Mbarawa.
Profesa Mbarawa amesisitiza kwamba Serikali imejipanga kudhibiti rushwa ili fedha nyingi zinazotumika katika miundombinu ilete matokeo chanya na kuwahakikishia kwamba ujenzi wa reli ya kisasa ya kati (Standard Gauge), itaanza baadaye mwaka huu na ikikamilika itapunguza gharama kubwa za usafirishaji zinazotumika kupitia malori.
Profesa Mbarawa amewashukuru wadau wa maendeleo kwa misaada mbalimbali wanayotoa katika sekta ya ujenzi wa barabara na ukarabati wa reli mara kwa mara na kusisitiza kwamba Serikali inatambua na kuthamini michango hiyo na kuomba washirikiane katika ujenzi wa reli ya kisasa ya kati (Standard gauge).
Zaidi ya kilomita 2600 za Reli ya Kisasa (Standard gauge) zinatarajiwa kujengwa kutoka Dar es Salaam-Morogoro-Dodoma-Tabora-Isaka hadi Mwanza ambayo ni uti wa mgongo wa reli hiyo.
Na Sehemu nyingine ni kutoka Tabora-Mpanda hadi Kalemela na Tabora-Uvinza hadi Kigoma ambayo itaunganisha na nchi za Rwanda na Burundi na hivyo kufungua huduma za kiuchumi na uchukuzi kati ya Tanzania na nchi za maziwa makuu.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano