Prof Mbarawa Awabana TEMESA Kivuko cha Kigamboni
Amesema takriban asilimia 20 ya abiria wanaotumia kivuko cha Mv Magogoni na Mv Kigamboni wanavuka bila kulipa nauli hali inayoathiri mapato stahiki ya kivuko hicho.
“Nawapa miezi mitatu muwe mmefunga mfumo kamili wa kupokea nauli wa elektroniki ambao utadhibiti ukwepaji wa kulipa nauli ili kuongeza mapato na kufikia shilingi milioni 25 kwa siku,” amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Waziri Mbarawa amesema nia ya wizara yake ni kukusanya mapato stahiki kutoka katika vivuko vyote ili kuwezesha kununua kivuko vipya na kukarabati vivuko vingine kadri iwezekanavyo.
Aidha ameagia ufanyike uboreshaji wa bwalo la kupumzikia abiria upande wa magogoni ili liweze kuhudumia watu wengi na katika hali nzuri na kuagiza uboreshaji huo kuanza mara moja.
Amezungumzia umuhumi wa wafanyakazi wa vivuko vya Magogoni na kigamboni kuwa na lugha nzuri kwa abiria wao na kuwasaidia wale wenye mahitaji maaalum ili kuboresha huduma ya usafiri ya vivuko hivyo.
Ameitaka TEMESA kuweka mfumo wa tiketi za msimu zitakazowezesha wafanyakazi kulipa kwa awamu moja au mbili kwa mwaka na hivyo kunufaika na punguzo maalum na kuondoa usumbufu wa kulipa nauli kila siku.
Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa TEMESA Eng. Prisca Mkama amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa mapato ya kivuko cha Magogoni yataimarika hivi karibuni kufuatia mikakati madhubuti wanayoifanya katika kuboresha huduma zao hususani eneo la Kigamboni.
Tariban abiria elfu 60 hutumia kivuko cha Mv. Magogoni na Mv. Kigamboni kuvuka kwa siku katika harakati za shughuli za kijamii na kibiashara.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO