WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa amewaagiza viongozi wa Serikali kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama na wananchi mkoani Singida kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria wananchi wanaohujumu miundombinu ya barabara na kuisababishia hasara Serikali.
Profesa Mbarara ametoa agizo hilo mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya yenye urefu wa Kilomita 89.3 kwa kiwango cha lami na kubaini kuwa baaadhi ya wananchi wameanza kuhujumu barabara hiyo.
“Tumepanga kujenga barabara ya Mkiwa-Itigi-Makongolosi kwa kiwango cha lami, sasa kitendo cha kuanza kuhujumu barabara iliyokwisha kamilika ni kitendo kisichokubalika na hatua kali zitachukuliwa kwa wote watakaobainika”, amesema Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesisitiza umuhimu wa kila mwananchi wa Mkoa wa Singida na Tanzania kwa ujumla kuilinda miundombinu ya barabara, reli na mawasiliano ambayo inajengwa kwa fedha nyingi ili idumu kwa muda mrefu.
“Tutaimarisha stesheni ya Itigi na kuimarisha mawasiliano ya simu ili kuwezesha eneo hili kuwa na mawasiliano ya uhakika na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Singida”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa mzani wa kupima magari katika eneo la Bumbuwa katika yabarabara ya Manyoni-Itigi-Chaya na kumtaka Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Singida Eng. Leonard Kapongo kuhakikisha ujenzi wa mzani huo unakamilika kwa wakati na magari yote yanayostahili yanapimwa.
Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Singida Eng. Leonard Kapongo amemhakikishiaProf. Mbarawakuwa ujenzi wa barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya yenye urefu wa kilomita 89.3 umekamilika kwa asilimia 98 na umehusisha makalvati makubwa 48 madogo 118.
Zaidi ya shilingi bilioni 109.6 zimetumika katika ujenzi wa barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya iliyojengwa katika mfumo wa usanifu na ujenzi ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya Manyoni-Itigi-Chaya-Nyahua hadi Tabora.
Serikali Kuwatumbua Wanaopokea Rushwa Kwenye Mizani
SERIKALI imesema itachuku hatua kali ikiwemo kumfukiza kazi na kumfikisha mahakamani mfanyakazi wa Mizani atakayebainika anajihusisha na vitendo vya kupokea rushwa ili kuruhusu magari kupita bila kupimwa uzito.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Eng. Joseph Nyamhanga wakati alipokagua huduma za upimaji uzito wa Magari katika Mzani wa Njuki Mkoani Singida. Alisema hadi sasa kuna baadhi ya wafanyakazi wa Mizani wameachishwa kazi kutokana na kujihusisha na vitendo vya kupokea rushwa kutoka kwa madereva wa magari ya Mizigo na abiria.
“Hatutasita kuchukua hatua kwa mfanyakazi yeyote atakayejihusisha na vitendo vya rushwa, hatua kali tutachukua dhidi yake ikiwemmo kumfikisha mahakamani”. Amesema Eng. Nyamhanga.
Badala yake Eng. Nyamhanga amewataka wafanyakazi wote wa Mizani nchini kufanya kazi kwa uadilifu kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa Mizani ili kuweza kuleta ufanisi katika vituo vya kazi.
Pia amewataka madereva wa magari na abiria nchini kushirikiana na Wizara hiyo kwa kutoa taarifa za Wafanyakazi wa Mizani wanaowaomba rushwa ili kuweza kuondoa kero hiyo kwa wananchi wanaotumia hudum za Mizani nchini. Vile levile amewaasa madereva wa magari ya mizigo kutozidisha uzito wa mizigo kwenye magari ili kuepusha uharibifu wa barabara ambazo hujengwa kwa kutumia kodi za wananchi.
“Madereva mnawajibu wa kulinda barabara hizi kwa kutozidisha uzito wa mizigo kwenye magari yenu ili kuziwezesha barabara zetu zidumu kwa muda mrefu”. Amesisitiza Eng. Nyamhanga.
Aidha, Eng. Nyamhanga amesema Wafanyabiashara na madereva wa magari makubwa ya mizigo yaendayo nje ya nchi kuchangamkia fursa ya kuwapo kwa stika maalum za magari hayo kwani kutapunguza idadi ya vizuizi vya upimaji wa uzito na hivyo kuharakisha safari zao.
Naye Msimizi wa Mzani wa Njuki Mnanka Chile amewaomba madereva wa magari kuzingatia sheria na kanuni za alama za barabarabi na kuwa makini pindi wanapokaribia seheme za Mizani ya kupimia uzito wa Magari.
Katibu Mkuu Eng. Josph Nyamhanga yupo katika ziara ya kukagua Miradi ya Ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, Vivuko na huduma za Mizani katika Mikoa ya Dodoma, Manyara Singida na Mara.
Imetolewa na kitenga cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.