WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ameipa muda mpaka mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu,Kampuni ya mawasiliano ya Halotel iwe imekamilisha Kazi ya kufunga mkongo wa intaneti katika shule tatu za kila wilaya hapa nchini.
Pia ameiagiza serikali mkoani Tanga kuifuatilia Kampuni ya mawasiliano ya Halotel kwa saababu imekuika taratibu za mkataba wake na serikali ambao alitakiwa kufunga mkongo wa mawasiliano ya intaneti kwenye shule tatu za sekondari kwa kila halmashauri ya wilaya lakini badala yake wamefunga Moderm ya 3G.
Amesema moderm hizo za 3G haziendani na kasi ya teknolojia inayotumika kwa sasa na kwamba kitendo hicho ni ukiukwaji mkubwa wa mkataba huo na serikali ambao waliwekeana mwaka jana.
Ametoa agizo hilo kwa kaimu mkuu wa mkoa wa Tanga, Abdulla Lutavi wakati alipokua akipokea taarifa ya mkoa ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake mkoani humo
“Lengo la pamoja ni kuona maendeleo ya sekta ninazosimamia za miundombinu ya ujenzi,uchukuzi na mawasiliano zinaimarika na kuwawezesha watanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025”, amesema Prof. mbarawa.
Amesisitza kuwa Serikali iliingia mkataba na Kampuni ya Halotel kwa makubaliano ya kufikisha huduma ya mawasiliano hasa vijijini na kuhakikisha inatoa huduma ya mtandao kwa ofisi za serikali wilayani na katika shule tatu katika kila wilaya jambo ambalo bado halijafanikiwa kwa kiasi kikubwa.
“Tumepata taarifa kwamba hapa Tanga kuna shule za Old Tanga, Mikanjuni na Maweni wamefungiwia moderm tena za 3G tofauti na makubaliano sisi mkataba unaeleza kutumia mkongo sasa inakuaje”,alihoji Waziri Prof. Mbarawa.
Katika hatua nyingine waziri Mbarawa ametembelea bandari ya Tanga na kuagiza kuanza kutumiwa kwa mfumo wa compyuta katika utendaji badala ya watu kutumia mfumo wa karatasi uliozoeleka ambao hauleti tija .
Amesema lengo la serikali ni kuhakikisha bandari inaongeza mapato kutoka takriban shilingi bilioni 600 mwaka uliopita hadi kufikia trilioni moja mwaka huu hivyo kusisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa kasi, weledi na kutumia mfumo wa kompyuta unaoleta uwazi.
Amewataka wananchi wa eneo la Mwambani kutakakojengwa badari ya Tanga waondoke katika eneo hilo mara moja kwani wameshalipwa fidia na hatua iliyobaki ni serikali kuliendeleza eneo hilo.
Ameiagiza Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), kufanya upembuzi yakinifu haraka ili kuwezesha ujenzi wa bandari hiyo kuanza mara moja.
“Bandari ndio moyo wa uchumi wa Tanzania hivyo fanyeni kazi kwa weleni,uadilifu,uwazi na kutumia mifumo ya kisasa ili matokeo makubwa ya uchumi yaonekane na Tanzania inufaike kwa fursa ilizonazo”, amesisitiza prof. Mbarawa.
Katika ziara hiyo Prof. Mbarawa amekagua utendaji kazi na kutoa maelekezo kwa kampuni ya simu ya TTCL,Posta,Mamlaka ya Viwanja vya Ndege TAA, Mamlaka ya Anga TCAA na Mamlaka ya hali ya hewa TMA na kusisitiza kufanya kazi kwa weledi na kufikia malengo.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO