Prof. Alexander Songorwa Ateuliwa Mkurugenzi Idara ya Wanyamapori

Prof. Alexander Nyangero Songorwa Mkurugenzi wa Wanyamapori

Na Mwandishi Wetu

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bi. Maimuna Tarishi amemteuwa Profesa Alexander Nyangero Songorwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori (Wildlife Division ) kuziba nafasi iliyokuwa wazi. Katibu huyo pia amemteuwa Profesa Jafari Ramadhani Kideghesho kuwa Mkurugenzi Msaidizi, kuongoza Sehemu ya Matumizi Endelevu ya Wanyamapori (Sustainable Utilisation of Wildlife Section).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam kwa vyombo vya habari na Msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii, George Matiko uteuzi huo uliofanywa na Katibu Mkuu, Bi. Tarishi ni kwa mamlaka aliyonayo kifungu cha 6
(1) (b) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002.

Akifafanua zaidi, Matiko alisema Profesa Songorwa, ni msomi fani ya Wanyamapori akiwa na shahada ya kwanza (B.Sc.) ya Sayansi katika Zoolojia na Ekolojia ya Wanyamapori aliyoipata Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (mwaka 1987),
na Shahada ya Uzamili (MSc) katika Mipango na Maendeleo Vijijini ya Chuo Kikuu cha Guelph, Ontario, Canada (1994).

Aliongeza kuwa Prof. Songorwa pia ana shahada ya uzamivu (PhD) katika Uhifadhi Maliasili ya Chuo Kikuu cha Lincoln, New Zealand (1999) na kabla ya kuteuliwa alikuwa Profesa Mshiriki katika Usimamizi wa Wanyamapori, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Morogoro. Pia ndiye aliyekuwa Mkuu wa Idara hiyo ya Usimamizi wa Wanyamapori SUA.

“Akiwa Wizarani Profesa Songorwa alihudumu katka nafasi mbalimbali zikiwemo Askari Wanyamapori, Mkuu wa Kanda na Msaidizi wa Mkuu wa Mradi katika Pori la Akiba la Selous. Pia alihudumu kama Ofisa Mwandamizi katika Mradi wa Uhifadhi Shirikishi wa Wanyamapori, Makao Makuu, Dar es Salaam,” alisema Matiko.

Aidha alisema kwa upande wake, Profesa Kideghesho si mgeni Idara ya Wanyamapori kwani kabla ya kujiunga na SUA mwaka 1999, alikuwa mwalimu wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka (CAWM-Mweka), Moshi kuanzia 1993. Aliongeza kuwa kitaaluma Prof. Kideghesho ana shahada ya kwaza (B.Sc.) katika Kilimo ya SUA (1993), Shahada ya Uzamili (MSc) katika Biolojia ya Uhifadhi ya Chuo Kikuu cha Kent, Uingereza (1996), na Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Norway kilichopo mjini Trondheim (2006).

Aliongeza kuwa kabla ya uteuzi huo Prof. Ramadhani alikuwa Profesa Mshiriki katika Usimamizi wa Wanyamapori katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Morogoro, huku akisisitiza kuwa utekelezaji kwa wateuliwa umeanza Septemba 24, 2012.