KLABU ya soka ya Simba ina furaha kubwa kuutangazia umma wa Watanzania kwamba imeingia mkataba na kampuni ya Prime Time Promotions/Clouds Media Group unaohusiana na Promosheni na Masoko (Promotion and Marketing) kwa ajili ya mechi ya Kombe la Shirikisho (CAF) kati ya Simba na Kiyovu Sport ya Rwanda.
Ushirikiano huo wa namna ya kipekee una lengo la kuhakikisha kuwa Watanzania wengi wanafahamu juu ya pambano hilo na wanahudhuria pambano hilo la kimataifa lakini pia kuweka mazingira ya kuvutia kwa makampuni na wafanyabiashara ili wawekeze katika mchezo huu kipenzi cha Watanzania.
Ingawa mkataba huu wa sasa baina ya Simba na Clouds unahusu mechi hii moja pekee, kuna kila dalili kuwa huu utakuwa mwanzo wa kampuni hizi mbili kufanya kazi kwa pamoja kwa muda mrefu kwa lengo la kuhakikisha mchezo wa soka unakua kwa faida ya taifa letu.
Kwa kuanzia tu, pamoja na mechi hii ya Kiyovu, Simba SC leo pia inatangaza kuanzisha kwa luninga ya klabu, Simba TV, ambayo lengo lake kubwa litakuwa ni kuonyesha shughuli za kila siku na matukio mbalimbali yanayohusiana na klabu yetu.
Clouds Media Group kupitia Clouds TV ndiyo watakaokuwa wakionyesha vipindi hivyo vya Simba mara moja kwa wiki mwanzoni lakini lengo ni kuwa na televisheni ambayo itakuwa inaonyesha habari za Simba saa 24 kila siku.
Ndiyo maana basi, sisi katika Simba, tunaamini kuwa ushirikiano huu baina ya Simba na Clouds unafungua njia ya maendeleo anuai katika kila nyanja inayohusiana na mchezo wa soka hapa nchini.
Simba SC inapenda kutumia fursa hii kukaribisha makampuni na wafanyabiashara kujitokeza kudhamini mchezo wa soka hapa nchini kwa vile uzoefu unaonyesha kuwa kuwekeza katika soka kunalipa.
Imetolewa na Geofrey Nyange, Makamu Mwenyekiti Simba SC