Na Anna Nkinda – Colombo, Sri Lanka
MKUTANO wa 22 wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola umefunguliwa leo mjini Colombo nchini Sri Lanka kwa mara ya kwanza na mtoto wa Malkia wa Uingereza, Price Charles bila ya kuhudhuriwa na Malkia Eizabeth wa Pili ambaye ni Mkuu wa Jumuiya hiyo.
Akiongea wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Mahinda Rajapaksa Theatre Prince Charles alisema viongozi hao wanakutana ikiwa ni mwaka mmoja tangu kusainiwa kwa makubaliano ya kuboresha utendaji kazi wa jumuia hiyo hivyo basi makubaliano hayo yawaongoze ili watakapokutana tena wasijadili changamoto zinazowakabili bali ni jinsi gani wameweza kufanikiwa.
Aidha atika mkutano kama huo wa mwaka 2011 uliofanyika mjini Perth nchini Australia Malkia Elizabeth alitangaza kuanzishwa kwa mfuko wa Diamond Trust Jubilee ambao utawanufaisha nchi wanachama wa Jumuia ya Madola. Tangu kuanzishwa kwa mfuko huo umeweza kuwafikia na kuwasaidia watu, mashirika, wafanyabiashara na Serikali za nchi wanachama.
“Kama mlivyosikia mfuko huu unafanya kazi kubwa mbili ambazo ni kutibu na kuzuia ili kuepukana ugonjwa wa upofu wa macho pia kuna programu mpya ya viongozi vijana inayotambulika kama Her Majesty’s Diamond Jubilee.
Miradi hii itasaidia kubadilisha maisha ya watu mamilioni katika nchi za Jumuia ya Madola ila haitaweza kufanikiwa kama nyinyi hamtaweza kushiriki na kuendelea kuunga mkono mipango yote hii miwili”, alisema Prince Charles.
Akiwakaribisha viongozi na wageni waliohudhuria mkutano huo Rais wa Sri Lanka Mahinda Rajapaksa alisema hivi sasa nchi nyingi Duniani zinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na hali ngumu ya uchumi na kuziomba nchi wanachama wa jumuia hiyo kujadili kwa pamoja jinsi gani wanaweza kukabiliana na hali hiyo katika nchi zao.
Rais Rajapaksa alisema, “Sisi nchi wanachama wa Jumuia ya Madola tuangalie jinsi tunavyoweza kujadili vitu vinavyozuia kuleta maendeleo kwenye nchi zetu katika mambo ya siasa na uchumi bila ya kuwasahau wanawake na watoto.
Hata kama suala la uchumi litachukua nafasi tusiwasahau watu wetu, mtaji wa kutosha wa mtu unaisaidia nchi kufanikiwa na kuweza kukuwa ni muhimu watu waweze kuwasiliana katika nchi wanachama na uweza kutimiza malengo yetu.
Mkutano huo ambao umeudhuriwa na wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa 41 kati ya nchi wanachama 52 akiwemo Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete aliyeambatana na mkewe Mama Salma Kikwete unafanyika katika nchi ya Sri Lanka iliyopo barani Asia ikiwa ni baada ya miaka 24 kupita tangu ufanyika kwa mkutano mkubwa kama huo.