MFALME Otumfuo Osei Tutu wa Pili wa Ufalme wa Ashanti nchini amewashauri baadhi ya Waafrika kuacha kuitumia demokrasia vibaya kwa kutowaheshimu viongozi wa nchi na Serikali za Bara hilo ambao amesema kuwa anaamini fika kuwa wamedhamiria kuimarisha demokrasia katika Bara hilo.
Mfalme huyo pia amewaambia Waafrika kuwa hali ya baadaye ya Bara la Afrika ni nzuri lakini mafanikio yote ya Afrika yatategemea jinsi Waafrika wenyeji wanavyoendesha nchi zao na wala siyo kutokana na sera za mashirika ya fedha duniani.
Aidha Mfalme huyo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete wamekubaliana kuwa Afrika ndilo Bara ambalo dunia nzima itakuwa inalikimbia katika siku zijazo.
Mfalme Otumfuo Osei Tutu wa Pili na Rais Kikwete amekutana leo, Jumapili, Julai 10, 2011, Ikulu, Dar es Salaam, mara baada ya Mfalme huyo kuwa amewasili nchini kuanza ziara ya siku 10 kwa mwaliko wa Rais Mstaafu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa.
Mara baada ya mazungumzo yao, viongozi hao wawili wamekula chakula cha mchana pamoja na Rais Mkapa na wawakilishi wachache wa familia zilizokuwa za kichifu nchini.
Mfalme amemwambia Rais Kikwete kuwa ni vizuri kuona maendeleo makubwa ya demokrasia katika Afrika na ari ya viongozi wa sasa kuimarisha demokrasia hiyo, lakini ni jambo la kusikitisha kuwa baadhi ya Waafrika sasa wameanza kuitumia vibaya demokrasia kwa kutoheshimu, na wakati mwingine, kudharau viongozi wa Afrika.
“Kiongozi wa nchi huchaguliwa na wananchi wote. Hivyo, ni muhimu kuwa baada ya uchaguzi kufanyika na kumalizika, wananchi wote, waliompigia kura na wale ambao hawakumpigia kura kuonyesha heshima inayostahili kwake kwa sababu yeye sasa ndiye kiongozi wa nchi,“ amesema Mfalme.
Katika mazungumzo yao, Mfalme na Rais kikwete pia wamekubaliana kuwa miaka ijayo dunia itakuwa inalitegemea Bara la Afrika katika kudumisha mafanikio ya kiuchumi duniani.
“Hali ya baadaye ya uchumi wa dunia itakuwa mikononi mwa Afrika. Changamoto ya Bara letu, kwa hiyo, ni jinsi gani ya kuweka akili yetu pamoja ili kuweza kubuni sera nzuri zinakazoendeleza matunda ya kiuchumi na kijamii ya Bara letu na zitakazoleta maisha bora kwa wananchi wetu. Mpira uko uwanjani mwetu lakini hali ya baadaye ya uchumi wa dunia ni katika Afrika,” amesema Rais Kikwete.
Mfalme amekubaliana na Rais akisema: “Afrika ndilo Bara linaloangaliwa na dunia nzima kwa sasa na katika miaka ijayo. Lakini mafanikio ya Afrika yako mikononi mwa sisi Waafrika wenyewe na wala kwenye mikono ya IFM (Shirika la Fedha Duniani) ama Benki ya Dunia.”
Viongozi hao wawili pia wamekubaliana kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Ghana, uhusiano ambao ulijengwa katika miaka ya mwanzo ya uhuru wa nchi hiyo kupitia viongozi wa mwanzo wa nchi hizo mbili, Mwalimu Julius Nyerere na Osagyefo Kwame Nkurumah ambao wote ni marehemu sasa. Nchi ya Ghana ilikuwa nchi ya kwanza Kusini mwa Jangwa la Sahara kupata uhuru, kutoka ukoloni wa Kiingereza, mwaka 1957.
“Nimefurahi sana kufika Tanzania. Nimesikia mambo mengi mazuri kuhusu nchi hii tokea wakati wa viongozi wetu Julius Nyerere na Kwame Nkurumah. Naamini kuwa ziara yangu itaanzisha jitihada kubwa zaidi za kuimarisha uhusiano kati ya nchi zetu mbili. Nimefurahi sana kufika Tanzania,” amesema Mfalme Otumfuo Osei Tutu wa Pili.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu
DAR ES SALAAM.