Pori Tengefu Haligawanywi -Pinda

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda

SERIKALI imetengua tamko lilitolewa Machi 19, mwaka huu na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki la kupunguza ukubwa wa pori tengefu la Loliondo kutoka kilometa za mraba 4,000 hadi kilometa za mraba 1,500.

Uamuzi huo umetangazwa juzi jioni (Jumatatu, Septemba 23, 2013) na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati akizungumza na wakazi wa kata nane za Tarafa ya Loliondo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenya uwanja wa michezo wa Wasso, wilayani Ngorongoro mkoani Arusha.

Waziri Mkuu alisema Serikali imefikia uamuzi huo baada ya kufanya vikao pamoja na mawaziri aliombatana nao na kukubaliana kuwa wakazi hao waendelee kuishi kama ilivyokuwa awali kabla tamko halijatolewa na Balozi Kagasheki.

“Nilikuja wilayani Ngorongoro ili nijionee hali halisi ya vijiji vinavyodaiwa kuondolewa. Nilitaka nione kuna miundombinu ya aina gani katika eneo husika na hasa huduma za jamii. Nimeona hali ya malisho, umbali uliopo kutoka vijijini hadi eneo tajwa, miundombinu iliyopo, niliuliza idadi ya kaya zilizopo… kuna kijiji nimeambiwa kina watu zaidi ya 9,000… kwa kweli nimeamini tembea uone!”

“Tumefikia uamuzi kwamba wakazi wa kata hizi zote, muendelee na utaratibu wenu wa awali wa namna ya kuendeleza eneo la Loliondo kana kwamba hilo tamko halipo,” alisema Waziri Mkuu na kuamsha makelele ya shangwe miongoni mwa wakazi wa Loliondo ambao wengi wao ni Wamasai.

Aliwataka waendelee na kamati za mahusiano ya kijamii zilizokuwepo baina ya vijiji na wawekezaji ziimarishwe. Pia alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Arusha aweke utaratibu wa kuitisha vikao kila baada ya miezi mitatu ili wadau wote wakae na kukosoana kila inapobidi.

Mara baada ya kuwasili Loliondo Jumapili asubuhi (Septemba 22, 2013) akitokea Arusha, Waziri Mkuu aliamua kutembelea vijiji vyote ambavyo viko kwenye ushoroba (corridor) wa kilometa za mraba 1,500 kando ya hifadhi ya Serengeti, Ngorongoro na Pori tengefu la Loliondo ambavyo wakazi wake walitakiwa kuhamishwa ili kulinda mazalia ya wanyamapori, kutunza mapito ya wanyama na vyanzo vya maji.

Vijiji hivyo ni Ololosokwan, Soitsambu, Kertaloo, Oloipir, Olorian Maiduguri, Losoito Maaloni na Arash. Alibakiza kijiji kimoja tu cha Piyaya kwa sababu kiko umbali wa km. 50 kutoka Arash na jua lilikuwa limekwishazama.

Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Arusha kwa ziara maalum ya kusikiliza matatizo ya ardhi yanayowakabili wakazi wa wilaya ya Ngorongoro, katika tarafa za Ngorongoro, Loliondo na Sale kabla ya kuhutubia mkutano huo aliamua kukutana na wadau wa maendeleo na wawakilishi wa asasi za kiraia zilizopo Loliondo pamoja na wazee wa kimila (Malaigwanan) na kusikiliza maoni yao kuhusu suala hilo.

Mbali ya kero hiyo ya wakazi kuhamishwa ili kupisha ushoroba, kero nyingine ambazo Waziri Mkuu alizipokea zilihusu ukosefu wa maji, ajira wa vijana na ukosefu wa barabara ya kudumu. Ili kutatua suala la barabara, Waziri Mkuu leo anaondoka Loliondo kwa njia ya barabara kupitia mto wa Mbu hadi Arusha ili ajionee hali ya barabara hiyo ambayo ni miongoni mwa ahadi za Rais Jakaya Kikwete.

Mawaziri aliokutana na kufanya kikao nao jana asubuhi ni Bw. William Lukuvi (OWM – Sera Uratibu na Bunge), Prof. Anna Tibaijuka (Ardhi na Maendeleo ya Makazi), Bw. Jumanne Majaliwa (Naibu Waziri TAMISEMI – Elimu), Bw. Lazaro Nyalandu (Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii), Dk. Binilith Mahenge (Naibu Waziri wa Maji), Bw. Benedict Ole Nangolo (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) na wabunge wa CCM ambao ni wajumbe wa Kamati ya Mwigulu. Nao ni Bw. Christopher Ole Sendeka, Bw. Lekule Laizer na Mary Chatanda. Wengine ni wataalamu wa wilaya ya Ngorongoro na kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Arusha.