Na Mwandishi wa Jeshi la Polisi- Zanzibar
JESHI la Polisi Zanzibar limewaagiza wamiliki na wafanyabiashara wa baa visiwani humo kuchukua tahadhari kwa kuweka walinzi imara katika maeneo yanayozunguuka nyumba za biashara hiyo ili kuepuka matishio ya uchomwaji wa baa zao.
Afisa Uhusiano wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, amesema kua tahadhari hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar, ACP Aziz Juma Mohammed, wakati wa hafla ya kutunuku vyeti vya sifa na kutoa zawadi kwa Askari Polisi waliozima matukio ya kihalifu na kukamata silaha.
Kamanda Aziz amesema kuwa matukio ya uchomaji baa yanaweza kuzuilika kama kila mfanyabiashara wa baa ataweka walinzi imara wanaoweza kukabiliana na watu wanaojichukulia sheria mkokononi kwa kuchoma moto nyumba za biashara za vileo.
Hata hivyo Kamanda Aziz amesema kuwa Jeshi la Polisi litaendelea na juhudi zake za kufanya doria za mara kwa mara katika maeneo mbalimbali na kutafuta taarifa za kiintelijensia ili kuwabaini na kuwakamata wale wote wanaojihusisha na vitendo vya uchomaji moto wa baa.
Kamanda Aziz amekiri kuwa ingawa kuna matukio ya moto yanayotokana na ajali za kawaida, lakini baadhi ya matukio ya uchomaji wa baa hufanywa kwa makusudi na watu wachache aidha kwa kutokana na imani zao za kidini ama visa mbalimbali.
Kamanda huyo amesema Jeshi la Polisi litaendelea kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kuwa wamekuwa wakishiriki katika vitendo hivyo kwani amesema wote wanachukuliwa kama wahalifu na kwa yeyote atakayekamatwa atafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Amewataka wananchi kutii sheria bila shuruti ili kuepuka madhara yanayoweza kuwapata kama mtu atakamatwa na kulazimishwa kuitii sheria aliyopaswa kuitii kwa hiyari yake.
Naye mmoja ya Maafisa wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Zanzibar amesema kuwa baadhi ya matukio ya moto katika majenyo mbalimbali yamekuwa yakisababishwa na hitilafu za umeme na kuachwa kwa mabaki ya moto kwenye majiko ya wafanyabiashara za vyakula.
Naye Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar Ahamada Abdallah, amewataka askari Polisi kuanza utekelezaji wa agizo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya uzuiaji wa matumizi ya mifuko ya plasitki kama sehemu ya utii wa Sheria bila shuruti.
Katika hafla hiyo zaidi ya Askari Polisi 10 wakiwemo Makachero, Polisi wa Usalama Barabarani na Askari wa wanaosimamia ulinzi na usalama katika maeneo ya shehia mjini Zanzibar wamepata vyeti vya heshma na zawadi ya fedha tasilimu kutoka kwa IGP.