Polisi Zanzibar, Vikosi vya SMZ Kufanya Matembezi ya Amani

Kamishna wa Polisi Zanzibar, CP Mussa Ali Mussa

Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi

JESHI la Polisi Zanzibar Jumamosi Juni 15, 2013 litafanya matembezi (Route March) ya pamoja kati yake na Askari wa Vikosi vya SMZ. Kamishna wa Polisi Zanzibar, CP Mussa Ali Mussa, ameyataja makundi mengine yatakayoshiriki kwenye matembezi hayo kuwa ni pamoja na, Vikundi vya Mazoezi ya Viungo pamoja na Vikundi vya Ulinzi Shirikishi.

Amesema matembezi hayo ambayo yataanza saa 12.00 alfajiri siku hiyo, yataanzia kwenye Viwanja ya Polisi Ziwani na kuishia nje ya Uwanja wa Michezo wa Amani saa 3.00 asubuhi.

Kamishna Mussa amesema matembezi hayo yenye sura ya amani yatapokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Maghari Unguja Bw. Abdallah Mwinyi Khamisi na washiriki wake watatoka katika mikoa mitatu ya Unguja.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya Habari, Kamishna Mussa amewaomba wananchi wa mji wa Zanzibar na Viunga vyake wameombwa kufika nje ya Uwanja wa Amani kuanzia saa 2.00 asubuhi ili kupata ujumbe utakaotolewa siku hiyo.

Viongozi mbalimbali kutoka Vyombo vya Ulinzi na Usalama Zanzibar watahudhuria katika mapokezi hayo. Aidha Waandishi kutoka vyombo mbalimbali wa Habari, wameombwa kuhudhuria ili kusaidia kutoa elimu kwa umma juu ya yale yote yatakayoelekezwa kwa manufaa ya Taifa letu.