KUFUATIA mlipuko wa bomu uliotokea katika mkutano wa Chama cha demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kuuwa watu wawili na majeruhi zaidi ya 60 katika mkutano huo, Jeshi la Polisi Nchini limeunda timu ya maofisa kutoka makao makuu Dar es Salaam ili kuongeza nguvu ya uchunguzi wa mlipuko wa bomu hilo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP. Said Mwema amesema imeteua maofisa hao ili kwenda kuongeza nguvu za uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo la mlipuko wa bomu uliotokea Soweto, Kata ya Kaloleni Arusha.
Alisema timu hiyo ya uchunguzi inayoenda kusaidiana na wengine kutoka Mkoani Arusha, inajumuisha makamishna wawili kutoka Operesheni na Idara ya Upelelezi Makao Makuu, itaongozwa na Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo, Paul Chagonja na Kamishna Issaya Mngulu kutoka Idara ya Upelelezi Makosa ya Jinai.
Jeshi la Polisi mbali na kulaani kitendo hicho ambacho kinaashiria vitendo vya kigaidi, linaendesha oparesheni nchini nzima ya kubaini wafadhili na wahusika wanaopanga matukio hayo ya kinyama.
Aidha IGP amewaomba wananchi wote wenye taarifa zozote juu ya tukio wawasiliane moja kwa moja na IGP Mwema kwa namba 0754 78 55 57 au katika kituo chochote cha Polisi.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi akizungumza leo amesema uchunguzi wa tukio hilo unahusisha vikosi vyote vya usalama nchi likiwemo Jeshi la Wananchi (JWTZ) kubaini wahalifu hao ambao wanatishia usalama wa nchi na raia wake.
Hii ni mara ya pili kwa mlipuko wa bomu la kurushwa unatokea Mkoani Arusha katika mkusanyiko wa watu kwani hivi karibuni ulitokea mlipuko mwingine wa bomu katika moja za Parokia za Kanisa Katoliki mkoni humo.