Na Mwandishi Wetu, Arusha
JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha limezuia mwaandamano ya amani ya waandishi wa habari mkoani hapa yaliopangwa kufanyika kwa nia ya kulaani mauaji ya mwandishi wa habari wa Kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi.
Taarifa ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD), Lotson Mponjoli, yenye namba AR/B. 5/VOL. II/75 kwa uongozi wa Chama Cha Waandishi Mkoa wa Arusha (APC), imesema wamezuia maandamano hayo kwa madai kupisha shughuli za kiserikali zinazoendelea mjini hapa.
“Napenda kuwajulisha kwamba ni vema mkasitisha maandamano yenu mliyoazimia kuyafanya, kwa kuwa wiki hii yote tutakuwa na shughuli za kiserikali kwani tutakuwa na ugeni mkubwa wa uongozi we Serikali kimataifa wanaohudhuria mkutano wa mazingira,”
“Pia tuna maandalizi ya mtihani wa darasa la saba, hivyo hakutakuwa na askari wa kutosha katika kulinda na kuongoza maandamano,” alisema na kuongeza katika taarifa hiyo. Alidai kuwa kutoka na serikali kuchukulia suala hilo la mauaji kwa uzito wake, hivyo wanahabari tuwe na subira kwa matokeo kwani Serikali kupitia tume iliyoundwa itatoa taarifa juu ya jambo hilo.
Awali Jeshi la Polisi lilizuia maandamano hayo ambayo yalipangwa kuanzia eneo yalipo Makao Makuu ya CCM, ambapo kabla ya kufika kwa polisi hao kundi kubwa la wanahabari wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali ya kulaani mauaji hayo. Aidha baadhi ya wanahabari walipinga vikali kitendo cha polisi kuzuia maandamano hayo kwa madai kwamba kuna uhaba mkubwa wa polisi wa kulinda maandamano, huku ikidaiwa pia kwa sababu ya ugeni mkubwa wa mkutano wa mazingira unaoendelea.
Walidai kuwa jeshi hilo halikupaswa kuzuia maandamani hayo kwani wajibu wao ni kupewa taarifa na kulinfa maandamano, ambapo pia walidai kuwa hawahitaji Polisi kuwalinda. Kwa upande wake Katibu wa (APC) Eliya Mbonea, akiwa ameambatana na baadhi ya viongozi wengine wa chama hicho walifika katika eneo hilo na kuwaomba wanahabari kutii amri hiyo iliyotolewa na Polisi.
Baada ya maelezo hayo, waandishi walilazimika kusitisha maandamano na kuondoka katika eneo hilo huu kukiwa na gari la polisi waliokuwa wakiongozwa na OCD, katika eneo hilo ambao nao waliondoka baada ya kusitishwa kwa maandamano hayo.