Askari Polisi wawili wa kituo cha Mgeta wilayani Mvomero mkoani Morogoro, wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kumpiga Diwani wa Kata ya Kiteo, Exavery Msambara, kwa madai kwamba amekuwa akihoji utendaji wa kazi za polisi.
Afisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Josephat Rugila, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo Desemba Mosi, mwaka huu saa 4:00 asubuhi katika kituo cha Polisi Mgeta, na kufafanua kuwa tayari limewaweka mahabusu askari hao kwa ajili ya hatua za kinidhamu za Jeshi la Polisi sambamba na kuwachukulia hatua baada ya uchunguzi kukamilika.
Rugila aliwataja askari hao kuwa ni G 1689 PC Majaliwa na F 3347 PC Abdallah, ambao alisema walikutana na diwani huyo maeneo ya karibu na kituo hicho cha polisi na kumsimamisha kwa madai kuwa kuna barua yake polisi hivyo aende kuichukua.
Kwa mujibu wa Rugila, diwani huyo akiwa na Diwani mwenzake wa Kata ya Langali, Cletus Lokoe, waliongozana hadi kituoni hapo.
Hata hivyo, alisema wakati wakiwa kwenye viti kusubiri barua hiyo, askari Abdallah alianza kumhoji Diwani Msambara kwanini amekuwa akihoji utendaji wa kazi za polisi badala ya kufanya kazi zake, jambo lililomfanya diwani huyo kuamua kuhoji kama ndicho alichoitiwa na kutaka kuondoka.
Rugila alisema inadaiwa kuwa askari huyo alimzuia diwani huyo na kuanza kumpiga mateke na ngumi na kwamba diwani alijaribu kukimbia kunusuru maisha yake bila mafanikio, kwani askari yule alimkimbilia na kumvutia ndani.
Alisema kutokana na hali hiyo, askari wengine waliokuwa katika eneo hilo, PC Mwajaliwa na Sajenti Tungaraza, walilazimika kuingilia kati kuamulia ugomvi huo wakishirikiana na diwani Lokoe.
Afisa huyo alisema wakati yote hayo yakitokea, mkuu wa kituo hicho hakuwepo kituoni na baada ya kurejea alikuta taarifa za tukio hilo na kuchukua hatua za kuwakamata askari hao na kuwaweka rumande na diwani huyo alipewa fomu namba tatu ya polisi kwa ajili ya kwenda hospitali kwa matibabu.
Rugila alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi zaidi wa tukio hilo na kama watuhumiwa hao watabainika kuwa na makosa watachukuliwa hatua kali zaidi za kisheria.
Mwishoni mwa wiki, Jeshi la Polisi mkoani Kigoma, lilitangaza kuwa linawashikilia askari wanane wa kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kasulu kwa tuhuma za kumtesa, kumpa kipigo na kumuua raia, Festo Andrea, kwa tuhuma za ujambazi wa kutumia silaha.
Askari hao wanadaiwa kumpiga kichwani na mbavuni kwa kutumia kitako cha bunduki na kumwekea miti sehemu zake za haja kubwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai, alisema askari wote wanane wanawashikilia na wanafanya uchunguzi dhidi yao na ikibainika watafukuzwa kazi na kupelekwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Kamanda Kashai alikataa kutaja majina ya askari hao kwa maelezo kuwa tuhuma hizo zinachunguzwa na kushughulikiwa na uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi na kwamba baada ya uchunguzi huo, yeye atapewa maagizo ili atoe taarifa kwa umma.