*Wengine wanne washikiliwa na Polisi
Janeth Mushi, Arusha
JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha limemuua mtuhumiwa anayesadikiwa ni jambazi, Pokea Samson Kaaya maarufu kama ‘Kaunda’ aliyekuwa akitafutwa na jeshi hilo baada ya kumuua askari namba F.2218, Konstebo wa Upelelezi Kijanda Mwandu kwa risasi ya shingo na kumjeruhi Mrakibu Msaidizi wa Polisi, ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arusha, Faustine Mafwele wiki iliyopita.
Katika tukio hilo upekuzi uliofanywa ndani ya nyumba hiyo
asubuhi yake, zilipatikana risasi 36 za SMG, risasi 12 za Shortgun, kitako 1 cha shortgun, mtambo wa bunduki hiyo ambayo ilikuwa imefunguliwa pamoja na soksi 2 za kuvaa usoni zinazotumiwa na majambazi hao.
Kamanda wa Jeshi la polisi mkoani Arusha, Thobias Andengenye
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea Januari 13 mwaka huu katika kijiji cha Orarash, kitongoji cha Lengine wilayani Arumeru mkoani hapa.
Andengenye alidai kuwa awali jeshi hilo kwa kushirikiana na wananchi mnamo Januari 6 majira ya saa4 asubuhi eneo la Moshono mtaa wa Lereta walifanikiwa kupata silaha alizotoka nazo jambazi huyo SMG iliyokuwa na namba 1016188011 na risasi zake 20 na magazine mbili huku shortgun hiyo model 88-12GA na risasi 4 zilizokuwa zimehifadhiwa ndani ya sulphate na kufichwa kwenye kichaka.
“Januari 13 mwaka huu majira ya saa nane usiku polisi walifika katika eneo la kijiji cha Orarashi baada ya kupata taarifa kuwa jambazi huyo alikuwa katika boma la Anna Loshilari na kuizunguka nyumba hiyo huku wakiilinda hadi asubuhi majira ya saa 06:45 asubuhi ambapo jambazi huyo alichomoka ghafla ndani ya boma hilo na kuanza kukimbia.” Alisema.
Aliongeza kuwa jambazi huyo anadaiwa kufika katika boma hilo kwa ajili ya kutibiwa kwa mganga awa kienyeji, jeraha alilijeruhiwa januari 3 katika mguu wake wa kushoto wakati alipotora polisi eneo la Shangarai.
Alidai kuwa askari waliokuwepo eneo la tukio walimkimbiza jambazi huyo umbali wa kilomita mbili, ambapo ghafla jambazi huyo alimgeukia na kumvamia askari No. E. 9912 D/C Wito na kumuuma kidole gumba na
kumjeruhi jicho la kushoto kwa lengo la kumnyang’anya silaha aliyokuwa nayo.
SACP Andenye alisema askari wenzake waliokuwa katika eneo hilo
walifanikiwa kumuokoa mwenzao na kumpiga risasi jambazi huyo ghafla na kuanguka na kufariki dunia kabla hajafikishwa hospitalini.
Aidha katika tukio hilo Jeshi hilo lilifanikiwa kumkamata Agness Silas (40) ambaye ni mke wa jambazi huyo ambao walitoroka polisi hao Januari 3, Josephat Haule (33), Juma Salum (46) na Daine Masawe (19) wote wakazi wa mjini hapa.
Alisema kuwa jeshi hilo linaendelea kuwatafuta washirika wenzake wa
ujambazi huku mmoja wao akifahamika kwa jina la Agusti Shine, huku
jeshi hilo likiendelea kuwahoji watuhumiwa hao waliokamatwa.
“Bado Polisi inawashukuru wananchi wote waliosaidia kutoa taarifa za wahalifu na tuaomba waendelee kutupatia taarifa hizo, ili waweze kukamatwa na kupunguza uhalifu,” aliongeza.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhio maiti katika hospitali ya mkoa ya Mt. Meru kwa uchunguzi wa kidaktari.