Polisi wamshikilia ‘askari’ aliyemtorosha ‘muuaji’

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP-Said Mwema

Moshi

ASKARI Polisi mwenye namba F. 4049 Pc Maneno wa kituo cha polisi kati mjini Moshi mkoani Kilimanjaro anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma za uzembe kazini hali iliyosababisha mtuhumiwa wa mauaji kutoroka.

Askari huyo anashikiliwa kwa uzembe wa kusababisha mtuhumiwa wa Kesi ya mauaji ya Mwendesha bodaboda katika kituo hicho cha Polisi kutoroka baada ya kumtoa Lock Up kwa lengo la kumwaga uchafu kwenye ndoo na kuchota maji ya kufanyia usafi.

Mtuhumiwa huyo ambaye alikiri kuhusika na mauaji ya mwendesha pikipiki maarufu kama bodaboda aitwaye, Genuine Aloyce kwa jina maarufu Chiluba alikamatwa na kikundi cha waendesha pikipii katika eneo la Njoro Manispaa ya Moshi akiwa na simu ya marehemu.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Absalom Mwakyoma alisema mtuhumiwa huyo alitoroka Machi 22 majira ya saa Nne na Nusu asubuhi katika kituo cha polisi kati Moshi baada ya kufunguliwa na askari mwenye namba F. 4049 Pc Maneno aliyekuwa zamu ili akamwage uchafu na kuchota maji ya kufanyia usafi.

Kamanda alisema mtuhumiwa huyo aitwaye Valentine Joachim Edward kwa jina marufu Valee alikwenda kumwaga uchafu na kuchota maji lakini wakati anarudi na ndoo za maji alizitupa chini na kuanza kukimbia na kutokomea maeneo ya Njoro.

Kwa mujibu wa Kamanda baada ya mtuhumiwa huyo kukamatwa na waendesha boda boda na kufikishwa katika kituo cha polisi kati aliandika maelezo ya Onyo na kukiri kuhusika na mauaji hayo akiwa na mwenzake aitwaye Tall wa mkoani Arusha. Kamanda alisema pia mtuhumiwa huyo alipelekwa kwa mlinzi wa Amani nako pia aliandika maelezo ya ungamo na kukiri kuhusika na tukio hilo.

Kutokana na tukio hilokamanda alisema Askari Na. F. 4049 Pc Maneno amewekwa Lock Up kwa uzembe akiwa kazini na kwamba juhudi za kumsaka na kumkamata mtuhumiwa huyo zinaendelea kufanyika.