Na Mwandishi Wetu, Arusha
JESHI la Polisi mkoani hapa, limedai kuwa ujumbe mfupi wa maandishi aliodai kutumiwa Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema umetumwa na mtandao wa simu toka nje ya nchi. Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Arusha Liberatus Sabas alidai kuwa uchunguzi wa awali kuhusu ujumbe huo unaodaiwa kutumwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo kwenye simu ya Lema Aprili Mwaka huu uchunguzi wa awali umeonesha haukutumwa kupitia kampuni yoyote ya simu za mkononi za hapa nchini.
Aidha ujumbe huo uliotumwa kwa Lema mwishoni wa mwezi Aprili ulisomeka “Umeruka kihunzi cha kwanza nitakuonyesha mimi ni serikali, ulikojificha nitakupata na nitakupa kesi inayoitaka mimi.” Sabas alisema kuwa ujumbe huo ulidaiwa kutumwa kutoka namba 0752960276 inayotumiwa na Mkuu wa Mkoa Mulongo kwenda kwenye namba 0764150747 inayotumiwa na Mbunge huyo.
Alisema kuwa kufuatia madai hayo Jeshi hilo lilianza uchunguzi kwa kuzingatia Mkuu huyo alikanusha kumtumia Lema ujumbe wa aina yoyote, uchunguzi uliohusisha kampuni ya simu ambayo mtandao wake ulitumika katika utumaji wa ujumbe husika.
Sabas alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ujumbe huo mfupi hakikuwa kampuni ya simu husika (hakuitaja) kwa vile ‘Centre Number’ iliyotumika kutuma ujumbe huo mfupi wa maneno ni 44780200332, ambayo siyo ya mtandao wa kampuni husika bali ni ya mtandao ulio nje ya nchi.
Kamanda Sabas aliongeza kuwa uchunguzi zaidi unaendelea ili kuweza kubaini chanzo cha ujumbe huo na atakayebainika kuhusika na ujumbe huo sheria zitachukuliwa dhidi yake.