HAKIMU mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, Charles Magesa amemuamuru Ofisa wa Kituo Cha Polisi mkoani hapa kutekeleza amri ya Mahakama ya kumkamata Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe kwa kushindwa kutii amri ya Mahakama.
Hakimu Magesa ametoa agizo hilo leo mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha wakati alipokuwa akitoa uamuzi wa dhamana dhidi ya watuhumiwa (7) ambao hawakufika mahakamani Mai 27, mwaka huu wala wadhamini wao.
Alisema kuwa Mbowe ameshindwa kutii amri ya Mahakama kama watuhumiwa wenzake pamoja na mdhamini wake hivyo amri hiyo itekelezwe mara moja na mshtakiwa na mdhamini wake kufikishwa mahakamani wakati wowote.
Awali hakimu huyo alikuwa ametoa maagizo ya kukamatwa kwa Mbowe pamoja na Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Philemone Ndessamburo ambapo baada ya kumaliza kutoa maelezo mdhamini wa Ndessamburo alijitokeza na kuieleza Mahakama kuwa Mei 30 mwaka huu alikuwepo mahakamani kumuwakilisha Ndessamburo.
Hata hivyo wakili wa upande wa utetezi, Method Kimomogolo, alipoulizwa juu ya uwepo wa mdhamini huyo Mei 30 mahakamani hapo alidai kuwa ni kweli alikuwepo ila kutokana na hofu alishindwa kujitokeza hadharani kumtetea mtuhumiwa.
“Mheshimiwa hakimu hapa mahakamani siyo mahali panapozoeleka, kwa hiyo napenda kuieleza mahakama yako kuwa, Reuben Ngowi ambaye ni mdhamini wa Ndessamburo alikuwepo mahakamani ila hofu ilimfanya ashindwe kujitokeza hadharani,” alidai Kimomogolo
Kufuatia maelezo hayo ya kuridhisha Magessa aliieleza mahakama kuwa imempa nafasi nyingine Mbunge huyo(Ndessamburo) aweze kuendeela na dhamana yake nje.
“Kesi hii ni ya jinai ila siku kesi itakapotajwa tena lazima mshtakiwa afike mahakamani kwani kuwepo katika vikao vya kamati za bunge ni majukumu yao ya kila siku kama watumishi walivyo na majukumu yao lakini wanapohitajika mahakamani hutii amri ya mahakama”alisema Magesa
“Suala la wewe kuwepo mahakamani Mei 30,silipingi kwani nilikuona ukimnong’oneza Wakili wa utetezi ila sikufahamu ni kitu gani ulichomweleza,ila kama unajua unamdhamini nani ulipaswa kuieleza mahakama”Hakimu alimsisitizia mdhamini huyo
Hata hivyo baada ya mahakama kupitia hoja za pande zote mbili(Utetezi, Serikali) mahakama imeridhia kuendelea kwa dhamana za watuhumiwa wengine ambao hawakufika mahakamani hapo Mei 27 mwaka huu.
Watuhumiwa hao ni pamoja na Katibu Mkuu wa Chadema Dk. Wilbroada Slaa, Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, mbunge wa Rombo Joseph Selasini amabye aliwakilishwa mahakamani hapo na mdhamini wake.
Wengine ni Mchumba wa Dk. Slaa Josephine Mashumbusi ambaye vyeti vya daktari viliwasilishwa mahakamani hapo pamoja na Aquline Chuwa.
Aidha Hakimu huyo alipinga madai ya wakili Kimomogolo kuwa baadhi ya watuhumiwa ambao ni wabunge walishindwa kufika mahakamani hapo baada ya mkanganyiko uliotokea baina ya mahakama na upande wa utetezi.
“Mbona Aprili 27 mwaka huu mdhamini wa Joseph Selasini alikuwapo mahakamani na alitoa taarifa za Selasini kwa yupo kwenye kikao kwenye kamati za Bunge, Bagamoyo na mahakama ikamuelewa,” alihoji hakimu
Kesi hiyo inayowakabili viongozi wa ngazi za juu wa CHADEMA na wafuasi wake inatarajwia kuanza usikilizwaji wa awali Juni 24 mwaka huu.