POLISI wa kike anayefanya kazi Kituo cha Polisi Ilala, Dar es Salaam amekamatwa jijini Mbeya kwa tuhuma za kuiba mtoto mchanga wa siku saba, Goodluck Salehe wilayani Kyela. Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alisema mtuhumiwa alikamatwa juzi saa 4 asubuhi eneo la Meta akiwa na mtoto huyo.
“Ni kweli tumemkamata askari wa Kituo cha Polisi Ilala, Dar es Salaam akiwa na mtoto aliyeripotiwa kuibwa Aprili 6, mwaka huu wilayani Kyela,” alisema Msangi.
Akifafanua alisema mtoto aliyeibwa alizaliwa Machi 30, mwaka huu na kupotea katika mazingira ya utatanishi Aprili 6, mwaka huu. Akifafanua kuhusu tukio la wizi, alisema mama wa mtoto anayeitwa Mboka Mwakikagile akiwa Kitongoji cha Sama A Kijiji cha Ibanda Kata ya Itope, Kyela alipigiwa simu na mwanaume ambaye mzazi mwezake anayeishi Kasumulu kwamba atafika shangazi wa mtoto kuwaona na ampokee na waende hospitali.
Alisema baada ya muda, Mwakikagile akiwa nyumbani kwa wazazi wake alimpokea mwanamke aliyejitambulisha kuwa ni dada wa mzazi mwenzake akiwa na begi la nguo za watoto.
Baada ya mazungumzo, mwanamke huyo alimshauri Mboka kumpeleka mtoto huyo kliniki ili akapate matibabu ya kinga jambo, ambalo mama wa mtoto aliliafiki. Mama wa mtoto alisema yeye na yule mwanamke waliondoka kwenda Zahanati ya Njisi Kasumulu na walipofika waliambiwa kununua daftari kwa ajili ya mtoto.
Alisema alikwenda kununua daftari na aliporejea hakumwona mwanamke aliyemwachia mtoto wake na alipouliza aliambiwa ameondoka na pikipiki. Kamanda Msangi alisema uchunguzi wa awali unaonesha mtuhumiwa huyo alikula njama na baba mzazi wa mtoto huyo ili kufanikisha kumuiba. Msangi alisema taratibu zinafanyika kumfungulia mashtaka na kisha kufikisha mahakamani askari huyo.
CHANZO; Mwananchi