POLISI nchini Ugandan wamevamia ofisi za magazeti kufuatia taarifa kwamba Rais Yeweri Museveni anamuandaa mwanawe wa kiume kumrithi urais. Taarifa zinasema vituo viwili vya Redio pia vilivamiwa limeandika Gazeti la Serikali la New Vision.
Wiki iliyopita magazeti ya Uganda yalidai kuwa zipo njama za kuwaua wale watakao pinga mpango wa Rais Museveni kumuandaa mwanawe kuchukua madaraka ya Uganda. Magazeti hayo yalidai kuwa mipango hiyo ya mauaji ilitolewa na Mkuu fulani wa Jeshi la Uganda.
Bwana Museveni, ambaye amekuwa madarakani tangu 1986, anatarajiwa kung’atuka uongozini mwaka 2016. Kwa muda mrefu kumekuwa na madai kwamba Museveni anamuandaa mwanawe Muhoozi Kainerugaba,ambaye ni brigadier jeshini kushikilia uongozi wa Uganda. Hata hivyo Serikali ya Museveni imekanusha taarifa hizo na kudai ni za uzushi.
Mwanawe Museveni Brig. Kainerugaba. Wiki iliyopita magazeti ya The Daily Monitor na Red Pepper, yalichapisha barua ya siri ikidai ilikuwa imeandikwa na Jeneral David Sejusa, ikitaka uchunguzi ufanywe kuthibitisha madai kwamba kuna mipango ya kuwauwa wote watakao pinga mipango ya Rais Museveni kumpachika mwanawe uongozini.
Uvamizi uliofanywa kwa magazeti na vituo vya polisi umeidhinishwa na Mahakama ya Uganda huku ukielezwa unalengo la kutafuta barua hiyo inayodaiwa kuandikwa na mkuu huyo wa Jeshi akifichua njama za mauaji. Vituo viwili vya Redio vinavyohusiana na Daily Monitor, Dembe FM na KFM, pia vilivamiwa na kuzimwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Daily Monitor Bwana Alex Assimwe aliiambia BBC kwamba chumba chao cha Habari kilivamiwa na polisi wapatao 50 waliojihami kwa silaha.
Lakini wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wanadai kuwa ikiwa barua ya Jenerali Sejusa ni ya kweli basi ni dalili kuwa kuna hali mvutano ndani ya jeshi huku ikidhaniwa kuwa wanajeshi wakongwe huenda wanapoteza uwezo kwa wanajeshi chipukizi wanaoongozwa na mwanawe Museveni Brigadia Kainerugaba.
Jenerali Sejusa ni mwanajeshi mkongwe aliyekuwa katika vita vya ukombozi uliyomuweka Rais Museveni madarakani mwaka 1986. Kwa mujibu wa taarifa za AP kamanda mmoja wa jeshi Jenerali Aronda Nyakairima amenukiliwa akisema kuwa Jenerali Sejusa kwa wakati huu anachunguzwa kutokana na barua anayodaiwa kuiandika.
-BBC