Polisi Tanzania Kupambana na Uhalifu Kisasa Zaidi kwa Mtandao

Mkurugenzi wa Kampuni ya kizalendo ya Kotes (T) Ltd, Max Komba (wapili kulia-waliosimama), akikagua uchimbaji mtaro kwa ajili ya kutandika nyanya za mfumo wa mawasiliano kwenye kituo cha Polisi Oysterbay, Dar es Salaam, jana, kuunganisha kwenye mkongo wa mawasiliano wa taifa. Kulia ni Mhandisi wa masuala ya ICT, Makao Makuu ya Polisi, Mosses Maganza na watatu ni mhandisi wa Kotes (T) Ltd, Mohamed Sibuga.

JESHI la Polisi nchini limechukua hatua za kujiimarisha zaidi katika kuukabili uhalifu kisasa zaidi kwa kuamua kuviunganisha vituo vyake vikubwa kwenye mtandao wa mawasiliano katika mkongo wa taifa.
Kufuatia hatua hiyo, ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano hayo ya kuunganishwa kwenye mkongo wa taifa wa mawasiliano, umeshaanza kwenye vituo vikubwa vya polisi katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Kilimanjaro, Zanzibara na jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, jana, Mkurugenzi wa Kampuni ya Kotes (T) Limited iliyopewa na jeshi la polisi kutengeneza mindombinu hiyo, Max Komba, alisema, ujenzi huo ulianza kwenye Kituo cha Polisi Kurasini, Chuo Cha Polisi Chang’ombe na Oysterbay ambako ujenzi wake ulitarajiwa kukamilika jana.
Komba alisema, kampuni yake imepewa kufanya kazi katika mikoa hiyo kwa wiki tatu, tangu ilipoanza Julai 27 mwaka huu kwa mujibu wa mkataba, na ujenzi unatakiwa ume imekamilika ifikapo Agosti 20 mwaka huu.
Likizungumzia mradi huo, Jeshi la Polisi kupitia msemaji wake, lilisema, mradi huo ukikamilika utasaidia jeshi hilo kupunguza gharama na muda mwingi ambao limekuwa likilazimika kutumia katika kufuatilia kumbukumbu katika kuwatambua wahalifu.
Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Senso, alisema, kupitia mtandao huo, vituo vilivyounganishwa vinaweza kupata taarifa na kuziona kwa wakati mmoja na kwa haraka zaidi,  jambo ambalo litawezesha kumbaini mhalifu haraka zaidi na kuwa na ushahidi wa kutosha baada ya kumnasa.
“Mradi huu ni miongoni mwa maboresho mengi tunayofanya katika jeshi la polisi ili kwenda na wakati. Hivyo baada ya kukamilisha kwenye vituo vyenye hadhi ya mikoa kipolisi, tunatarajia pia kushuka hadi ngazi za wilaya kulingana na mahitaji”, alisema.