Moshi
MTU mmoja aliyefahamika kwa jina la Thomas Fosian (28), maarufu kama ‘Mlay Fundi’ mkazi wa Chekereni, Kahe mkoani Kilimanjaro anashikiliwa na Polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kumchuna mbwa kwa madai kwamba alitaka kula nyama yake.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Absalom Mwakyoma amethibitisha kukamatwa kwa Fosian na kudai amekamatwa, majira ya saa tisa alasiri eneo la chekereni ya Mabogini wilayani humo akiwa tayari ameshamchuna mbwa huyo huku akitaka kutaka kumla.
Mwakyoma amesema siku ya tukio askari mgambo walipewa taarifa kutoka kwa uongozi wa kijiji kuwa, Fosian akiwa nyumbani kwake alimkamata mbwa wa nyumbani kwao na kumchinja kisha kumchuna ngozi kwa nia ya kumchemsha kama supi.
Kwa mujibu wa kamanda uongozi wa kijiji kwa kushirikiana na wananchi wa Chekereni walimkamata mtu huyo na kumhoji kutokana na tukio hilo na kusema kuwa alimchinja mbwa huyo ili kunwa supu yake lakini uongozi wa kijiji ulishindwa kuelewa kama kweli alitaka kunwa supu au kuuzia watu.
Hata hivyo uongozi wa kijiji hicho ulipata mashaka na mtu huyo na kuweza kumfikisha katika kituo cha polisi Moshi kwa mahojiano zaidi ambapo askari baada ya kumhoji walibaini kuwa anamatatizo ya akili.
Kamanda alisema bado Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linaendelea na mahojiano na mtu huyo ili kujua kwa undani dhamira yake ya kumchinja mbwa huyo. Kamanda Mwakyoma anatoa wito kwa wananchi mkoani humo kuchukua tahadhari kwa watu wanaochinja wanyama kwa kificho ili kubaini aina ya wanyama wasiolika na kila jamii kutokana na kwamba mbwa huyo baada ya kuchunwa ngozi anaonekana kama mbuzi.
Hata hivyo wakizungumza na gazeti hili baadhi ya wakazi wa mji wa Moshi walisema kuwa kwa sasa kunapaswa kuchukuliwa hatua za makuzudi za kukagua wanaochoma nyama maarufu kama mishkaki kutokana na kwamba kama mbwa huyo anafanana na Mbuzi watu wanaweza kuchomewa na wakadhani ni nyama ya Mbuzi.