Pogba Aingia Kwenye Orodha ya Wachezaji Ghali Duniani

pogb

Paul Pogba amesema huu “ndio wakati bora zaidi wa kurejea Old Trafford” baada yake kukamilisha kuhamia Manchester United kwa kununuliwa £89m kutoka Juventus, ambayo ni rekodi mpya ya dunia.

Kiungo huyo wa kati mwenye umri wa miaka 23 amerejea miaka minne baada ya kuondoka United na kwenda Juventus kwa £1.5m mwaka 2012.

Pogba, ambaye ametia saini mkataba wa miaka mitano, ameongeza, “Hii ndiyo klabu bora kwangu kutimiza kila kitu ambacho kimekutumainia.”

Meneja Jose Mourinho amesema mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa huenda akawa nguzo ya klabu hiyo kwa mwongo mmoja ujao.

United watalipa mabingwa hao wa Italia euro 105m kumchukua Pogba, pamoja na nyongeza euro 5m (£4.5m) ambayo ni bonasi kwa kutegemea mafanikio yake pamoja na gharama nyingine.

Bei yake imezidi ya mshambuliaji wa Wales Gareth Bale aliyenunuliwa £85m kuhamia Real Madrid kutoka Spurs mwaka 2013.

Pogba alijiunga na United mara ya kwanza kutoka kwa klabu ya Le Havre ya Ufaransa mwaka 2009 akiwa na miaka 16, na akawachezea mechi chache kabla ya mkataba wake kumalizika Julai 2012.

Amecheza Juventus 178 na kuwafungia mabao 34 na kuwasaidia kufika fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya 2015.

Klabu hiyo ya Serie A ilikuwa imeahidi kumpa mkataba mpya. Real Madrid nao pia walitaka kumnunua.

Wachezaji walionunuliwa ghali karibuni
 2013 – Gareth Bale £86m (Tottenham Hotspur hadi Real Madrid)
 2009 – Cristiano Ronaldo £80m (Manchester United hadi Real Madrid)
 2009 – Kaka £56m (AC Milan hadi Real Madrid)
 2001 – Zinedine Zidane £46m (Juventus hadi Real Madrid)
 2000 – Luis Figo £37m (Barcelona hadi Real Madrid)