Pingamizi la kesi ya Lema latupwa

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema

Na Mwandishi Wetu, Arusha

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Arusha, imetupilia mbali pingamizi zilizotolewa na wakili wa Serikali, Timon Vitalisa na Method Kimomogolo anayemtetea mdaiwa ambaye ni mbunge wa Arusha Mjini (CHADEMA), Godbless Lema ya kutaka kufutwa kwa kesi ya kupinga uchaguzi wa mbunge huyo kutokana na kesi iliyofunguliwa dhidi ya Mbunge huyo na wananchi watatu na wakazi wa Arusha Mjini.

Akitupilia mbali pingamizi hizo jana, Jaji anayesikiliza kesi hiyo
Aloyce Mujulizi, alisema kuwa mahakama imeona hoja zilizotolewa katika
kesi hiyo ambazo ni pamoja na kutaka kufutwa kwa shauri hilo kwa madai kuwa kesi hiyo haikupaswa kufunguliwa na wapiga kura bali lilipaswa kufunguliwa na Dk. Batilda Burian aliyekuwa mgombea wa kiti hicho kupitia CCM, kwani yeye ndiye alipaswa kulalamika kutokana na
kudhalilishwa wakati wa kampeni.

Wapiga kura hao waliofungua kesi hiyo ni Musa Nkanga, Agness Mollel na Happy Kivuyo ambapo hoja nyingine walizowasilisha mawakili hao ni
haki ya msingi ya waleta madai kuruhisiwa kisheria kupeleka pingamizi
ya matokeo ya uchaguzi, ambapo walidai kwua mpiga kura hana haki
kisheria kuleta pingamizi.

Aidha katika kesi hiyo wadai hao pia wanadai kuwa Lema wakati wa
kampeni alimdhalilisha kijinsia Dk. Batilda Burian kwa kutoa lugha za
matusi ambapo Mrema anadaiwa kutoa lugha hizo katika vituo 22 tofauti
vilivyokuwa vinatumika katika mikutano ya kampeni za uchaguzi mwaka
jana, na kuongeza kuwa Lema alitoa lugha za kashfa na ubaguzi wa kidini na kijinsia ziliathiri matokeo ya uchaguzi katika jimbo hilo hali iliyosababisha mgombea huyo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushindwa kuchaguliwa.

Jaji huyo alisema mahakama hiyo imetupilia mbali hoja zilizotolewa na
Mawakili hao kutokana ana hoja hizo kutokukidhi vigezo kisheria na badala yake vimelenga katika mambo yasiyoijikita katika kesi hiyo na kuwaagiza wawalipe fidia kutokana na kushindwa kwa hoja zao walizozitoa awali na kuwaagiza leo mawakili hao wapeleke vielelezo mahakamani hapo juu ya fidia ya pingamizi za awali.

Baada ya Jaji, Mujulizi kutoa uamuzi huo wakili wa wadai Alute Mughwai na Modest Akida waliiomba mahakama kuongeza muda wa usikilizwaji wa kesi ya kupinga matokeo ya Ubunge kwani kesi hiyo ilianza kusikilizwa Septemba 9 na hadi hivi sasa imebaki miezi miwili na kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi kesi hiyo inabidi iishe Desemba mwaka huu.

Alute aliieleza mahakama hiyo kuwa kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi
kifungu cha 115 kifungu kidogo cha 2, kinachosema kuwa mahakama
itasikiliza na kuamua kesi ya uchaguzi kutoka tarehe ya kesi ya
malalamiko ilipowasilishwa mahakamani, ambapo kesi hiyo ilifunguliwa
Novemba 30 mwaka jana na kuanza kusikilizwa Septemba 9 mwkaa huu
kutokana na Serikali kujipanga.

Kutokana na hali hiyo wakili huyo aliiomba mahakama hiyo kuandika barua kwa Waziri wa Sheria na Katiba ili aweze kuongeza muda wa kesi hiyo hadi Juni mwakani kwani ikipangwa kusikilizwa kwa haraka haitawezekana na kunaweza kutoka udhuru wowote.

Alisema muda wa miezi miwili uliobaki ni mdogo na kesi hiyo haiwezi
kusikilizwa na kukamilika, na kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi kifungu
cha 115 (5) cha sheria ya uchaguzi kinachosema kwua endapo malalamiko hayana uwezekani wa kukamilika Waziri wa Katiba na Sheria ana uwezo wa kuongeza miezi mingine sita (6) ili kesi iweze kukamilika na kutolewa uamuzi.

Jaji Mujulizi alisema ataangalia uwezekano wa kesi hiyo kuongezewa
muda kwa kuwasiliana na Waziri wa Katiba na Sheria na kuahirisha kesi
hiyo hadi kesho kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.