Pingamizi kesi ya madiwani Chadema zasikilizwa

Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe

Na Janeth Mushi, Arusha

HAKIMU wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, Hawa Mguruta amekubali kusikiliza pingamizi la wadaiwa ambao ni Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe katika kesi iliyofunguliwa na madiwani watano kupinga kufukuzwa uanachama.

Aidha pingamizi hizo zilizotolewa kwa njia ya maandishi na wakili upande wa wadaiwa, Method Kimomogolo zinaeleza kuwa Mbowe hawezi kushtakiwa binafsi, CHADEMA haiwezi kushtakiwa kwa jina lake, Maombi ya kufukuzwa uanachama yamepitwa na wakati kwani madiwani hao walishakata rufaa Baraza Kuu la Chama hicho na Mahakama haina uwezo wa kusikiliza ksi hiyo bali Mahakama Kuu ndio
yenye uwezo.

Katika kesi hiyo ya madai yenye namba 17/2011 iliyofunguliwa Agosti 10 mwaka huu ambapo madiwani John Bayo, Ruben Ngowi, Charles Mpanda, Rehema Mohamed na Etomii Mallah ilipinga kufukuzwa uanachama wao na kuomba mahakama kutoa amri ya zuio la muda kwa Chadema kutofanya mikutano ya hadhara na kuwataja majina au kuwadhalilisha kwa namna yoyote ile.

Hakimu Mguruta alikubali kusikiliza pingamizi hizo kutoka kwa wadaiwa lakini upande wa wadai wakili wao, Linda Bosco aliiomba mahakama kuwapa muda wa siku 14 ili waweze kuwasilisha pingamizi zao mahakamani hapo kwani jana walishindwa kuziwasilisha kutokana na wakili mwenzake, Severine Lawena kusikiliza kesi nyingine mahakama Kuu kwajaji Aisha Nyerere.

Hakimu Mguruta alisema kutokana na ombi la wakili Bosco na kwamujibu wa barua aliyopokea hakutaja kumbukumbu imeonyesha kuwa wakili Lawena alikuwa kwenye kesi nyingine tatu kwa Jaji Nyerere lakini haikufafanua kama kesi hizo ni zadharura kama kesi hiyo ya kupinga madiwani hao kufukuzwa uanachama.

Alisema kutokana na Lawena kutofafanua vizuri alitoa muda kwa wakili huyo upande wa wadai kuwasilisha pingamizi zao kwanjia ya maandishi Septemba 12 mwaka huu kabla ya saa 7:00 mchana na Septemba 13 pingamizi hizo zitaanza kusikilizwa.

Awali kabla ya Hakimu Mguruta kutoa uamuzi huo wakili upande wa wadaiwa, Kimomogolo alidai Mawakili upande wa wadai wanapoteza muda kwani kesi ya kupinga kuvuliwa uanachama ilifunguliwa kwa dharura hivyo ni bora kesi hiyo ikasikilizwa kwa dharura na si mawakili hao kukubali kesi nyingine wakati wanajua kuwa kesi hiyo ilifunguliwa kwa dharura.