WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Serikali za Mitaa ambayo mwaka huu Kitaifa yatafanyika katika mji wa Sumbawanga mkoani Rukwa.
Kilele cha maadhimisho hayo ni tarehe Mosi Julai na sherehe za maadhimisho hayo zinaanza kesho Juni 24 nchini kote.
Akizungmza na waandishi wa habari jana,Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Hussein Kattanga alisema kuwa maadhimisho hayo ambayo yalianza rasmi nchini mwaka 2005 yana lengo la kuwahabarisha wananchi juu ya umuhimu wa Serikali za Mitaa,nafasi na wajibu wao kwa Serikali za Mitaa.
Pia kuwahimiza wananchi kuhusu utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini.
“Serikali iliamua kutenga siku maalum kwa ajili ya kuadhimisha siku ya Serikali za Mitaa kila mwaka,siku hiyo ni tarehe 01Julai ya kila mwaka,lengo la maadhimisho haya ni kuwahabarisha wananchi juu ya umuhimu wa Serikali za Mitaa ,nafasi na wajibu wao kwa Serikali za Mitaa,pia kuwahimiza wananchi kuhusu utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa lengo la kuchochea ukuaji wa Uchumi na kupunguza umasikini.”alisema Katibu Mkuu huyo
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo siku hiyo inatoa fursa kwa kila Halmashauri kuonesha shughuli mbalimbali zinazotekelezwa katika Mamlka hizo na kwamba hii inafanyika katika ngazi zote za Mamlaka za Serikali za Mitaa,yaani vitongoji,Vijiji,Mitaa,Kata na Halmashauri.
Alisema siku ni fursa muhimu kwa wnaanchi kuhoji Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu masuala muhimu uanayowahusu ikiwa ni pamoja na kutoa kero zao ,kuhoji uwajibikaji wa Halmashauri zao kwa miaka iliyopita na kutoa mapendekezo yao juu ya uendeshaji wa Mamlaka hizo kwa miaka inayofuata.
“Kupitia vyombo vya habari,napenda kuwaambia wananchji hii ni siku muhimu kwao kwani wanaweza kuhoji mambo mbalimbali ikiwemo utendaji wa Mamlaka hizo (Halmashauri) kwa miaka iliyopita lakini pia wanaweza kutumia fursa hiyo kuhoji na kutoa mapendekezo kwa Mamlaka hizo kwa miaka miaka ijayo.”
“Siku hiyo pia hutoa fursa kwa wananchi kujikumbusha kuwa Serikali za Mitaa ni vyombo vyao wenyewe wanavyotakiwa kuvitumia katika kujiletea maendeleo na kujenga mshikamano miongoni mwao.”