Pinda:Hata wanyama hawafanyi ushoga

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda

Dodoma

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amezungumzia sakata la Uingereza kutishia kuinyima misaada Tanzania kama haitaruhusu ndoa za jinsia moja, akisema, “haiwezekani, kwa kuwa hata wanyama hawafanyi hivyo.”

Alisema kama ilivyoelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Tanzania ipo tayari kukosa misaada ya Uingereza iwapo kigezo cha kupata misaada hiyo, ni nchi kuruhusu ndoa za jinsia moja.

Waziri Mkuu Pinda alitoa kauli hiyo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Chadema, Regia Mtema katika Kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.

Katika swali lake hilo, Mtema alitaka kusikia kauli ya Serikali kuhusu msimamo huo wa Uingereza uliotolewa na Waziri wake Mkuu David Cameroon na kujua endapo Tanzania imeshaanza kujipanga kuikataa misaada ya nchi hiyo.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, hivi karibuni tumesikia Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameroon akisema ili tupate misaada yao, tukubaliane na suala la ndoa za jinsia moja. Nini kauli ya Serikali? Je kama taifa, tumeshaanza kujipanga kuikataa misaada hiyo?,”alihoji Mtema.

Akijibu swali hilo Pinda alisema,”Kauli ya Serikali ilishatolewa na Waziri Membe mwenye dhamana na kurudiwa mara kadhaa na mawaziri wengine. Mimi sina kauli nyingine labda nitoe maoni yangu tu.”

Aliongeza; “Niseme tu kuwa mimi nakubaliana na msimamo huo wa Tanzania kwani, hata wanyama hawafanyi hivyo.”

Kauli ya Waziri Mkuu Pinda imekuja wiki chache tangu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe alipotoa msimamo wa Serikali kuhusu suala hilo, ambapo alisema kwamba Tanzania ipo tayari kukosa misaada yote kutoka Serikali ya Uingereza na kamwe haiwezi kuruhusu sheria inayotambua mashoga na kuhalalisha ndoa za jinsia moja.

Msimamo huo mzito wa Serikali umekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, kutamka kwamba nchi yake ina mpango wa kusitisha misaada yake kwa nchi ambazo sheria na katiba zao, hazitambui mashoga na ndoa za jinsia moja.

Cameron alikaririwa akithibitisha kuwa tayari amewajulisha juu ya suala hilo Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola waliokuwa wakihudhuria mkutano wa Jumuiya hiyo uliomalizika siku nne zilizopita, mjini Perth, Austaralia ambao pia ulihudhuriwa na Rais Jakaya Kikwete.

Waziri Mkuu huyo kutoka chama cha Conservative ambacho kilishinda uchaguzi Mei mwaka jana, alisema suala hilo la mashoga na ndoa za jinsia moja, ni moja ya mambo yanayoongoza sera ya Serikali yake kuhusu misaada kwa mataifa mbalimbali na kwamba tayari imeanza kutekelezwa katika maeneo kadhaa duniani.

Kauli ya Cameron imechukuliwa kama kielelezo cha ukoloni mamboleo ambao Uingereza inajaribu kuupandisha daraja kwa mataifa yanayoendelea kwa kigezo cha misaada. Lakini, Waziri Membe alisema pamoja na umasikini wake, Tanzania kamwe haitaruhusu upuuzi huo kwa kigezo cha misaada.

“Tanzania ni nchi maskini, lakini hatutakubali kuruhusu upuuzi huo eti kwa sababu ya misaada na fedha zao, lakini ushoga si utamaduni wetu, hata sheria zetu zinakataa,” alisema Membe.

Alifafanua kuwa katika kuonesha msimamo wa kutokukubaliana na masharti hayo, Tanzania imeshikilia msimamo thabiti kupinga upuuzi huo ambapo Januari mwaka huu, ilimkataa balozi shoga ambaye aliteuliwa na nchi yake kuja kuiwakilisha hapa nchini. Hata hivyo Waziri Membe hakutaja jina la balozi huyo wala nchi anayotoka.

“Niwape siri moja ambayo tuliificha lakini leo ngoja niwaambie, mwanzoni mwa mwaka jana nililetewa barua kunijulisha ujio wa balozi mmoja anayekuja kuiwakilisha nchi yake, mwanamume mwenye ndoa ya jinsia moja. Nilikwenda kumweleza Rais Jakaya Kikwete kuhusu wasifu wa balozi huyo mtarajiwa naye akajibu kwa maneno matatu, yarabi toba! Mkatae!,” alisema Membe.

Waziri Membe alifafanua kuwa serikali ilimkataa balozi huyo kwa kuwa ni kinyume cha utamaduni wetu na sheria za nchi kuwa na watu wenye tabia hizo.

Alisema alimjulisha Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo kwamba balozi huyo haruhusiwi kuja kufanya kazi nchini kwa kuwa ni kinyume na utamaduni wetu. “Waliendelea kuniomba kwamba balozi huyo akija hatatoka kwenye makazi yake akiwa na mwenza wake hivyo watu hawatamuona lakini tulimkataa kabisa, wakatuelewa.”

Alieleza kuwa tamko hilo la Waziri Mkuu Cameron linaweza kusababisha hatari ya kuvunjika kwa uhusiano miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola na koloni mama Uingereza na waziri huyo atabeba lawama hizo. Kwa mujibu wa Waziri Membe Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 kifungu cha tisa, kinatambua ndoa ya jinsia mbili tofauti, yaani mume na mke.

“Sheria hizi tunazozitumia hivi sasa tumezirithi kutoka Uingereza ambako leo wanatukuza ndoa za jinsia moja na ushoga,” alisema Membe.

Suala la kile kinachoitwa haki za binadamu kuhusu ushoga ilikuwa moja ya ajenda ambazo viongozi kadhaa walishindwa kuafikiana katika mkutano Perth. Hoja ya kukomesha vizuizi dhidi ya ushoga na ndoa za jinsi moja lilikuwa moja ya mapendekezo yaliyokuwamo katika ripoti ya ndani kuhusu matarajio ya baadaye ya Jumuiya hiyo ya Madola.

-CHANZO: Mwananchi