PINDA: TUNAHITAJI KUBAINI KILIMO CHA UMWAGILIAJI KINACHOTUFAA

Na Irene Bwire

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema kilimo cha umwagiliaji kitainua uzalishaji wa chakula nchini lakini inabidi Serikali ijipange kubaini ni aina gani ya teknolojia inahitajika katika kilimo hicho.

Ametoa kauli hiyo Mei 27, 2011 akizungumza na ujumbe wa kampuni ya Jain Irrigation Systems Ltd kutoka India, alipokutana nao ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam. Kampuni hiyo ina nia ya kuwekeza nchini katika eneo la umwagiliaji maji.

Waziri Mkuu alisema Tanzania ina fursa kubwa sana ya kuzalisha chakula kwa wingi kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji lakini inakwama kwa sababu ya kukosa teknolojia sahihi za kuendesha kilimo hicho.

“Inabidi tujipange kuangalia ni aina gani ya kilimo cha umwagiliaji maji na inatumia teknolojia ipi ambayo itafaa kwa ajili ya nchi yetu… ziko za aina nyingi lakini njia ya umwagiliaji wa matone inaweza kutufaa zaidi sababu haipotezi maji mengi,” alisema.

Alisema Tanzania inatarajia kupata wa masharti nafuu kutoka India ambao kama alisema utakuwa na manufaa zaidi ukitumika kwa ajili ya kujenga uwezo kwa kutoa mafunzo kwa wahandisi wa maji hasa katika teknolojia mpya na za kisasa zaidi. “Pia tutaangalia na uboreshaji wa miundombinu ya umwagiliaji itakayoendana na teknolojia

Aliwashukuru wawekezaji hao na kuwasisitiza waangalie matumizi ya teknolojia za kisasa lakini nafuu kwani Serikali imelenga wakulima wadogo na Watanzania wenye kipato cha chini ili waweze kuinua kiwango chao cha uzalishaji.

Mapema, akitoa taarifa fupi kuhusu kampuni yao kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi wa Masoko wa Jain Irrigation Systems Ltd ya India, Bw. Atul Jain wamejikita zaidi katika masuala ya uhandisi kama sehemu ya kuinua uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Alisema wataweka mifumo ambayo itawasadia wakulima waweze kuifahamu teknolojia ya umwagiliaji kwa kutoa mafunzo kila mara ili wasiwe tegemezi kwa kampuni hiyo pindi kunapotokea hitilafu za mitambo yao.

Kuhusu aina bora ya kilimo cha umwagiliaji, Bw. Jain alisema umwagiliaji wa matone unafaa zaidi kwa sababu kinachohitaji maji ni mmea na siyo shamba zima. “Uzuri wa kilimo cha umwagiliaji wa matone, unapata mazao bora zaidi na uzalishaji unaongezeka. Takwimu zinaonyesha kiwango cha uzalishaji kinapanda kutoka asilimia 50 hadi asilimia 250,” alisema.

Alitumia fursa hiyo kumweleza Waziri Mkuu kwamba wakulima wa Tanzania wanaweza kutumia fursa ya kilimo cha umwagiliaji kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya jamii ya mikunde kwani yana soko kubwa sana nchini India.

“Mahitaji ya mazao ya mikunde yamepanda kwa sababu matumizi yake yameongezeka… cha msingi ni kutumia fursa hii kuzalisha mazao ya kiwango cha juu yatakayoweza kumudu soko la kimataifa”, alisema.

Viongozi wengine aliofuatana nao Bw. Jain katika msafara wake ni Makamu wa Rais wa kampuni hiyo anayeshughulikia Biashara ya Nje na Huduma za Kiufundi; Bw. Lar Sharma, Bw. Shanjay Sethi (mwakilishi wao wa Nairobi, Kenya) na Bi Rupa Suchak ambaye ni mwakilishi wa kampuni hiyo hapa nchini.