WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali ya Tanzania haitaingia gharama zozote wakati meli ya Poisedon itakapokuwa inafanya uchunguzi wa mafuta na gesi katika pwani ya Tanzania.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Alhamisi, Julai 07, 2011) mara baada ya kutembelea eneo la viwanda vya kujenga meli (ship building area) ili kuona hatua mbalimbali za ujenzi wa meli na kuikagua meli ya uchimbaji mafuta iitwayo Poisedon ambayo inajengwa katika bandari ya Geoje, iliyoko kusini mashariki mwa Seoul, mji mkuu wa Korea Kusini.
Waziri Mkuu anatarajiwa kuizindua meli hiyo kesho (Ijumaa, Julai 8, 2011) saa 4 asubuhi katika bandari ya Geoje.
Amesema hivi sasa wanachofanya, wataalamu kutoka kampuni ya Petrobas ya Brazil ni kufanya utafiti na kubainisha maeneo mawili ambako meli hiyo itachimba endapo matokeo yatakuwa mazuri. “Tunaishukuru Serikali ya Brazil kwa kuamua kuisadia Serikali ya Tanzania kufanya utafiti huo muhimu,” alisema Waziri Mkuu Pinda.
Alisema hatua hiyo ni dalili njema kuwa uwekezaji unawezekana kufanyika Tanzania na kuahidi kuwa Serikali ya Tanzania itafanya kila iwezalo kuweka ulinzi wakati wataalamu hao wakiwa kazini ili kuzuia hatari ya kupambana na maharamia.
Mapema, akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu kuhusu ujenzi wa meli hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni Petrobas Tanzania Limited, Bw. Samuel Miranda alisema wanatarajia kwamba meli hiyo itafanya kazi katika ukanda wa pwani kwa muda wa miezi 20 na wamebaini maeneo mawili kati ya Mafia na Mtwara ambako meli hiyo itafanya kazi.
Kuhusu uendelezaji wa miundombinu, Bw. Miranda alisema hadi sasa wameshawekeza kiasi cha dola za marekani milioni 11 na ifikapo Desemba, 2011 watatoa dola za marekani milioni 14 ili kuendeleza bandari ya Mtwara.
Kuhusu utoaji ajira kwa Watanzania, alisema wameanza kutoa mafunzo kwa vijana 50 wa kike na wa kiume wa kutoka Mtwara ambao wakifaulu watafanya kazi katika meli hiyo.
“Meli hii itakuwa Mtwara na tunatarajia kuanza kazi mwanzoni mwa Septemba… tumeanza na vijana 50 kuanzia Julai mosi, watapewa mafunzo maalum ya miezi mitatu ya umeme na umakenika kuhusiana na masuala ya uchimbaji mafuta na si kitu kingine,” alifafanua.
“Mafunzo haya yanaendeshwa kwa ubia baina ya TPDC, VETA, Petrobas na taasisi ya CENAI ya Brazili ambayo inafanana na VETA ya hapa Tanzania, nia yetu ni kupata wakufunzi ambao wataendelea kufundisha vijana wengi zaidi katika fani hii…,” alisema.
Mbali na hatua hiyo, Bw. Miranda alisema wana mkataba na wahandisi wanne wa Kitanzania ambao tayari wamepelekwa Brazil kwa mafunzo ya muda mfupi na kisha watapelekwa Uingereza ili kujifunza zaidi masuala ya uchimbaji mafuta.
Naye Meneja Mradi wa kampuni ya Ocean Rig ya Uingereza ambayo inasimamia ujenzi wa meli hiyo, Bw. David Gray alimweleza Waziri Mkuu kwamba kwamba meli hiyo yenye urefu wa mita 242 na upana wa mita 52, imegharimu dola za marekani milioni 800.
“Meli hii ni ya nne, meli mbili zilishakwenda Brazil; ya tatu ni Mykonos itakwenda Brazil na hii ya nne ya Poseidon itakwenda Tanzania… meli hii ina uwezo wa kuweka vitanda 217, ina huduma za matibabu, recreational facilities ili watu watakaokuwa kazini waweze kumudu maisha katika bahari kuu,” alisema.
Alisema meli hiyo ina uwezo wa kuchimba kina cha futi 10,000 (sawa na mita 3,000) kutoka kina cha juu cha maji. Pia meli hiyo ina deki ya helikopta ambapo helikopta yenye tani 10 inaweza kutua.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Jenerali Mstaafu, Robert Mboma alisema ana imani kubwa na kampuni hiyo na zaidi ni katika kuongeza ajira kwa Watanzania.
Leo mchana, (Alhamisi, Julai 7, 2011) Waziri Mkuu atatembelea kiwanda cha kusindika bidhaa za baharini (marine products processing factory) kilichopo katika mji wa Geoje. Kesho asubuhi atazindua meli ya Poseidon na kuhutubia washiriki wa hafla hiyo na mchana siku hiyo atatembelea eneo la Georim lenye viwanda vya kusindika mazao ya kilimo katika mji huu wa Geoje.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu amefuatana na mkewe Mama Tunu Pinda, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Balozi wa Tanzania nchini Japan, Bibi Salome Sijaona, Mwenyekiti wa TPDC, Jenerali Mstaafu, Robert Mboma na viongozi waandamizi wa Serikali.
Waziri Mkuu anatarajiwa kuondoka Korea Kusini kesho kutwa jioni na kisha kurejea Dodoma kuendelea na ratiba za Bunge.