Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda amekutana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein Ikulu ndogo Migombani na kumpa pole kutokana na ajali ya kuzama kwa meli ya Spice Islanders hapo juzi alfajiri.
Waziri Pinda akiwa amefuatana na baadhi ya Mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwemo Mhe. Wilium Lukuvi na Mhe. Mery Nagu alimpa pole Dk. Shein pamoja na wananchi wote kutokana na tukio hilo na kuwataka wananchi kuendelea kuwa na subira katika kipindi hichi kigumu cha msiba.
Aidha, Waziri Mkuu Pinda, alitoa shukurani kwa kazi kubwa ya uokozi iliyofanywa na vikosi vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na wananchi na kueleza kuwa juhudi zao zimepelekea kuokolewa wananchi wengi.
Nayo Kamati ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoshughulikia Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ikiongozwa na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Edward Lowasa nayo ilifika Ikulu ndogo Migombani kumpa mkono wa pole Rais Dk. Shein.
Mhe. Lowasa akiwa na Wajumbe wa Kamati hiyo alimueleza Dk. Shein kuwa wameupokea kwa masikitiko makubwa msiba huo na ndio wakaona haja ya kufanya ujio wao huo kwa lengo la kutoa mkono wa pole kwa Mhe. Rais pamoja na wananchi wote. Waziri Mkuu huyo Mstaafu nae alipongeza juhudi kubwa zilizochukuliwa za uokozi na hatimae kupatikana baadhi ya wananchi.
Nao Wazee wa Chama Cha Maapinduzi walifika Ikulu Migombani kwa ajili ya kumpa mkono wa pole Rais Dk. Shein kufuatia msiba huo mkubwa wa Taifa. Wazee hao wa CCM, walimtaka Mhe. Rais kuwa na subira na kumtaka kuendelea kuwa wastahamilivu kwani msiba huo umewagusa watu wote.
Walieleza kuwa tukio hilo limeonesha mshikamano mkubwa uliopo kutokana na vikosi vyote vya ulinzi kushirikiana kikamilifu pamoja na wananchi katika uokozi tokea alfajiri ya siku ya tukio. Naye Rais Dk. Shein alitoa shukurani kwa ujio wa viongozi hao pamoja na wazee wa chama kwa nyakati tofauti kumpa mkono wa pole na kueleza kuwa msiba huo ni mkubwa kutokea hapa Zanzibar.
Katika mazungumzo yake Dk. Shein alieleza kuwa juhudi kubwa zimefanya na vikosi vya Ulinzi vya SMZ na vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na wananchi hasa wananchi wa Nungwi wakiwemo wavuvi, meli binafsi, Shirika la Bandari na kutoa shukurani kwa juhudi zao hizo.
Dk. Shein alisisitiza na kurejea kauli yake aliyoitoa wakati akitoa taarifa kwa wananchi hapo juzi kutokana na tukio hilo la kuzama kwa meli kuwa Serikali ya Mapindyuzi Zanzibar imeamua kuunda Tume ya uchaguzi ili kupata kujua chanzo cha tukio hilo na baada ya hapo taarifa rasmi itatolewa kwa wananchi pamoja na kufuatia taratibu za kisheria.
Alieleza kuwa idadi ya waliopatikana hadi jana mchana walikuwa 816 ambapo waliopatikana hai ni 619 na waliokufa ni 197 ambapo miongoni mwa waliokufa 39 walizikwa na Serikali na 158 walipata jamaa zao. Pia alieleza kuwa wengi ya wale waliopelekwa hospitali za MnaziMoja na Kivunge wamepewa ruhusa isipokuwa kijana mmoja ambaye anasumbuliwa na kikohozi amepelekewa Hospitali ya Muhimbili.
Akieleza utaratibu uliotumika katika mazishi hayo yaliofanyika huko Kama kuwa ni kila mmoja alizikwa katika kaburi lake kwani yalichimbwa makaburi ya kutosheleza. Alieleza kuwa leo serikali imeifanya ni siku ya mapumziko ili kuwapa wananchi muda mzuri wa kushiriki katika shughuli ya hitma na dua maalum ya kuwaombea wale wote waliopoteza roho zao katika msiba huo, hitma inayosoma jioni hii huko katika viwanja vya Maisara, mjini Unguja na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kitaifa.
Dk. Shein alieleza kuwa juhudi kubwa zimefanywa na Kamati ya Maafa, na ametoa shukurani kwa viongozi wote wa SMZ na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wameshiriki kikamilifu katika msiba huo akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.
Aidha, Dk. Shein alieleza kua tayari timu ya waokoaji kutoka Afika ya Kusini imeshawasili Zanzibar kwa ajili ya kusaidia shughuli za uokozi.
Pia, alivipongeza vyombo vya habari kwa ushiriki wao mkubwa na kueleza kuwa vyombo vya habari vimefanya kazi kubwa ya kutoa taarifa kwa wananchi sambamba na hayo, alieleza kuwa tayari washirika wa maendeleo zikiwemo nchi mbali mbali na mashirika ya Kimataifa wameonesha nia ya kusaidia.
Wakati huo huo Salam za rambi rambi zinaendelea kutolewa kwa Rais Dk. Shein kufuatia tukio hilo ambapo Ubalozi wa Tanzania Abudhabi na Consulate ya Tanzania Dubai UEA wameeleza kushtushwa sana na kuingiwa simanzi kubwa baada ya kupata taarifa ya tukio hilo.
Balozi Mohamed Maharage Juma kwa niaba ya wafanyakazi wenzake walitoa salam za rambi rambi, kwa Dk. Shein, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wananchi wote wa Zanzibae kwa msiba huo mzito uliotokea.
Nae Balozi wa Tanzania nchini Japan Salome Sijaona kwa niaba ya wafanyakazi wa Ubalozi huo wametuma salamu za rambi rambi kwa Dk. Shein na kueleza kuwa wanawapa pole wale wote waliopoteza ndugu zao katika ajali hiyo na kuwaomea kupona haraka kwa wale waliopo hospitali.