Pinda: BRN ni Nguzo ya Mageuzi Kiutendaji

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akijadiliana na mmoja wa viongozi wa maabara ya sekta ya afya, Dk. Linda Ezekiel baada ya kupewa maelezo kuhusu moja ya maeneo manne ya sekta ya afya yanayopendekezwa kuingizwa katika mfumo maalum wa utekelezaji wa miradi wa BRN.

Mtendaji Mkuu, Ofisi ya Rais-Usimamizi wa Utekelezaji wa Miradi (PDB) inayosimamia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), Omari Issa akimpongeza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda mara baada ya Waziri Mkuu kutoa hotuba ya kufunga maabara ya wiki sita ya BRN iliyokuwa ikijadili miradi ya sekta ya afya.

Sehemu ya viongozi wakifuatilia hotuba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipokuwa akifunga maabara ya afya jijini Dar es Salaam (Ijumaa). Maabara hiyo iliyokaa kwa wiki sita ilikuwa ikijadili miradi ya sekta ya afya itakayoingizwa katika mfumo maalum wa utekelezaji wa miradi wa BRN.

Na Mwandishi Wetu
 
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesema kuwa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ni chachu ya kuleta mageuzi katika utendaji na utekelezaji wa miradi nchini. Waziri Mkuu aliyasema hayo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki alipokuwa akifunga maabara ya sekta ya afya.
 
BRN ni mfumo maalum wa utekelezaji wa miradi ulioanzishwa na Serikali ya Tanzania Julai mosi, 2003 kwa lengo la kuweka vipaumbele katika miradi michache ya kitaifa itakayotekelezwa kwa haraka na yenye matokeo makubwa kwa watu. Akiuchambua mfumo huo, Pinda alisisitiza kuwa BRN inaleta utendaji wa haraka unaoachana na mfumo wa mazoea katika kuwapatia wananchi maendeleo.
 
Aliongeza kuwa msingi mwingine wa mafanikio ya BRN ni kupeana taarrifa na kuweka muundo wa usimamizi na ufuatiliaji unaohakikisha kuwa malengo yaliyowekwa yanafuatwa na mafanikio yanaonekana kwa haraka kwa wananchi.
 
Mfumo wa BRN unahatua nane zinazohakikisha kuwa miradi inayochaguliwa kutekelezwa chini ya mfumo wa kipaumbele inatekelezwa kwa wakati, ufanisi na bila kuiingiza Serikali katika gharama kubwa za uendeshaji.
 
“Mfumo wa BRN unasisitizia katika ufuatiliaji wa karibu ili kupata ufanisi mkubwa na kwa gharama ndogo. Nimefurahi kuambiwa hapa kuwa katika vikao hivi vya maabara ya BRN watu walikaa wiki sita za kufanyakazi kizalendo bila kulipwa posho,” alisema Waziri Mkuu na kutamani hali hiyo iendelee hadi katika hatua za utekelezaji.
 
Moja ya hatua nane za utekelezaji wa BRN ni mfumo wa maabara. Maabara ni mkusanyiko wa wataalamu wa sekta husika ambapo hukaa kwa pamoja kwa muda wa wiki sita, kuchambua maeneo yanayopaswa kufanyiwakazi ili yatekelezwe kwa haraka.
 
Katika maabara aliyoifunga Waziri Mkuu Pinda, takribani wataalamu 120 walikusanmyika kuchambua na kupendekeza miradi ya sekta ya afya itakayoingizwa katika BRN. Tayari BRN ina sekta nyingine saba za awali ambazo ni maji, nishati, elimu, kilimo, uchukuzi, ukusanyaji wa mapato na uboreshaji wa mazingira ya biashara.
 
“Katika maabara hii wataalamu mbalimbali wa afya walikusanyika kuchambua kwa kina maeneo ya kipaumbele yanayopaswa kuingizwa katika miradi ya afya katika BRN,” alisema Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashid.

Alisema maabara hiyo imesaidia wataalamu hao kuchambua matatizo mengi ya sekta ya afya na kuweza kubaini mbinu za kufanya ili kutatua kero za wananchi.