Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesisitiza kuwa uwekezaji katika wilaya ya Mpanda na Mkoa mzima wa Rukwa ni wa lazima na hauwezi kuepukika kama kweli wakazi wake wanataka kuondokana na umaskini.
Ametoa kauli hiyo leo mchana Septemba 10, 2011 wakati akizungumza na wakazi wa Wilaya ya Mpanda kwenye uzinduzi wa tawi la Benki ya CRDB, mjini Mpanda, mkoani Rukwa. Kabla ya kuzinduliwa tawi hilo, wakazi wa Mpanda walikuwa wakipata huduma kutoka Sumbawanga ambako ni umbali wa km. 240.
Amesema kumekuwa na vijimaneno kuhusu uwekezaji katika wilaya ya Mpanda na hasa maeneo ya Katumba lakini akatumia fursa hiyo kuwahakikishia mamia ya wakazi waliohudhuria uzinduzi wa tawi hilo kwamba hakuna mtu atakayeuziwa ardhi kwa sababu ardhi ni mali ya Serikali.
“Ndugu zangu wana Mpanda njia pekee ya kututoa hapa tulipo ni kupitia uwekezaji kama ambavyo mikoa mingine imefanya na ikaweza kusonga mbele kimaendeleo…tunahitaji wawekezaji wa ndani na wa nje katika kuleta maendeleo,” alisema.
“Mikoa ya Kilimanjaro, Morogoro na Kagera kuna wawekezaji wakubwa, wenzetu wana viwanda, watoto wao wanapata ajira katika viwanda hivyo lakini hakuna anayesema. Sisi hapa hata kiwanda cha kusaga unga tu hatuna, sasa iweje kualika wawekezaji huku kwetu linakuwa jambo linalokuzwa kiasi hicho?” alisema huku akishangiliwa.
“Hoja hapa siyo nani kauziwa ardhi bali ni nani anataka kuwekeza… Hakuna atakayeuziwa ardhi kwa sababu ardhi ni mali ya Serikali. Tunachofanya ni kuwakodisha, na utaratibu unajulikana miaka 33, 66 au 99 kutegemeana na jinsi mlivyojipanga,” alisema.
Alisema ametembelea nchi mbalimbali na ameona maendeleo yaliyopatikana kutokana na uwekezaji mkubwa cha msingi ni namna ya kuwaunganisha wawekezaji hao na wakulima wadogo ili waweze kunufaika na uwekezaji huo.
Mbali ya maeneo ya Katumba kulikokuwa na kambi ya wakimbizi, Waziri Mkuu aliyataja maeneo mengine yanayofaa kwa kilimo kuwa ni mapori yaliyoko njia ya kutoka Mpanda hadi Karema, Mpanda hadi Mwese na Rwila hadi Sikonge.
“Benki ya CRDB ina uwezo wa kutoa mitaji, nawasihi ndugu zangu kopeni katika benki na limeni ili tuzalishe ziada ya chakula na tuondokane na huu umaskini. Sasa hivi tuna wilaya 56 katika mikoa 15 ambazo zinakabiliwa na njaa, nahangaika kusafirisha mahindi kutoka Sumbawanga hadi mikoa ya Kaskazini ili watu wasife na njaa… hatuwezi kukaa hivihivi wakati ardhi tunayo. Hakuna nchi iliyofanya hivyo halafu ikasonga mbele,” alisema.
Alisema mbali ya kilimo, mkoa huo una fursa kubwa ya viwanda katika uvuvi na mifugo. “Mwaka 2005 tulikuwa na ng’ombe 10,000 tu, sasa hivi wako 219,779; mbuzi walikuwa 18,173 sasa hivi tunao 105,063…soko kubwa la nyama ng’ombe liko DRC, la mbuzi liko Uarabuni ni lazima tuwe na kiwanda cha kusindika nyama ili iweze kusafirishwa huko,” alisema.
Mapema, Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB, Bw. Martin Mmari alimkabidhi Waziri Mkuu hundi ya sh. milioni 10 zikiwa ni mchango kwa ajili ya Mkutano wa Uwekezaji wa Ukanda wa Ziwa Tanganyika utakaofanyika wilayani Mpanda Oktoba 17, mwaka huu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk. Charles Kimei akiwahutubia wakazi hao alisema katika siku zisizozidi 20 tangu lianze kutoa huduma kabla ya uzinduzi rasmi, tawi hilo limelwishafungua akaunti 1,000 ambazo ni wastani wa akaunti 100 kwa siku.
Alisema tawi hilo ni la 73 kufunguliwa hapa nchini ikilinganishwa na matawi 19 yaliyokuwepo wakati benki hiyo ikianzishwa mwaka 1996. Vilevile, alisema wana mobile ATM 10 zinazotoa huduma katika maeneo yaliyo mbali na wananchi.
Alisema benki hiyo imekwishatoa mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 300 kwa wateja wadogo na kwamba inajihusisha na asasi za kifedha 485 katika nchi nzima. “Kwa Mpanda peke yake, tumetoa sh. bilioni 16, lakini wateja walilazimika kwenda Sumbawanga,” alisema.
Waziri Mkuu anatarajiwa kurejea jijini Dar es Salaam Jumapili, Septemba 11, 2011.