Pinda awataka wazazi nchini waache uongo

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amewataka wazazi wenye uwezo wa kulipia watoto wao katika Vyuo Vikuu waache kusema uongo kwani kwa kufanya hivyo wanawakosesha watoto wa maskini kupata mikopo wanayostahili.

Ametoa kauli hiyo leo Novemba 5, 2011) wakati akiwahutubia washiriki wa mahafali ya pili ya Chuo Kikuu cha St. John’s yaliyofanyika kwenye chuo hicho mjini Dodoma.

Jumla ya wahitimu 1,002 walitunukiwa vyeti, stashahada, shahada na stashahada za juu katika fani za theolojia, uuguzi, famasia, sayansi na ualimu, biashara, uhasibu na fedha, masoko na teknolojia ya habari na mawasiliano.

“Bado kuna malalamiko nayapata kupitia njia mbalimbali kuhusu utaratibu wa Bodi ya Mikopo hasa pale watoto wa maskini, tena waliofaulu vizuri wanapokosa mikopo. Nawasihi wazazi wenye uwezo waache kusema uongo kwa sababu si busara kuwatumia watoto wao kupata mikopo wakati watoto wanaostahili wanaikosa…,” alisema.

Alisema wazazi wakiwa wakweli na kuamua kuwalipia watoto wao, fursa za watoto maskini kupata mikopo zitaongezeka. Alitumia fursa hiyo kuzungumzia changamoto zinazoikabili Serikali katika kukabiliana na kasi ya ongezeko la watu na kuonya kuwa linaleta changamoto kubwa katika utoaji wa huduma za jamii.

“Ongezeko la watu liko juu sana na kasi yake haioani na ukuaji wa uchumi… ukuaji huu unaathiri sana nyanja nyingi hasa elimu na ndiyo maana tunakabiliana na ongezeko la wanafunzi wanaoomba mikopo katika Bodi ya Mikopo kila mwaka,” alisema.

Alikitaka Chuo Kikuu kikuu cha St. John’s kiweke mikakati maalumu ya kusomesha wanataaluma wake wenyewe kwa sababu utaratibu wa kuazima wanataaluma kwa njia moja au nyingine unawakwaza wanafunzi kwani hawapati muda wa kutosha wa kuwasiliana na mwalimu wao.

”Nawasihi muongeze bidii ya kusomesha wanataaluma wenu kwa kasi ile ile ya kuongeza wanafunzi katika vyuo vyenu. Kama Taasisi inayojitegemea hamna budi kusomesha wataalam wenu wenyewe kwa msaada wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu,” alifafanua.

Akitoa wosia kwa wahitimu, Waziri Mkuu alisema: “Ombi langu kwenu ni kuwa, mkatumie elimu mliyoipata hapa chuoni kwa manufaa yenu, jamii na Taifa kwa ujumla. Msianze kwa kujifikiria nafsi zenu, kwani huo ni mwanzo wa tamaa, uchoyo, dhuluma, rushwa na pengine wizi.”

”Kwa sasa wapo Watanzania wengi wanajifikiria wenyewe, wamekuwa na tamaa hasa ya mali bila kuwafikiria Watanzania wenzao. Uzalendo unapungua. Hili naweza kusema ndilo chimbuko la maovu yaliyomo kwenye jamii yetu kama wizi, rushwa, ufisadi na hata mauaji yakiwemo mauaji ya walemavu wa ngozi. Kwa mwenendo huu hatuwezi kusonga mbele kiuchumi wala kijamii. Tunahitaji kubadili mwelekeo. Nanyi ni wadau muhimu katika kubadili mwelekeo wa jamii yetu,” aliwaasa.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wahitimu hao, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Balozi Paul Rupia alisema Chuo hicho kina mpango wa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Witwatersrand cha Afrika Kusini katika kuimarisha mafunzo ya shahada ya famasia.

Alisema chuo hicho pia kimejipanga kuanza ujenzi wa madarasa na bweni jipya litakalochukua wanafunzi wa kike 800 mapema mwaka ujao.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Eginald Mihanjo alisema hii ni mara ya kwanza kwa chuo hicho kutoa Shahada ya Uuguzi na Famasia. Waliohitimu uuguzi ni 150 na famasia ni 29.

Kuhusu changamoto zinazokikabili chuo hicho, Prof. Mihanjo alisema wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa rasilmali fedha, uhaba wa mabweni na uhaba wa wanataaluma.

Alisema ziko baadhi ya fani za sayansi ambazo baadhi ya wazazi wanashindwa kumudu kuwalipia watoto wao. Aliiomba Serikali iwasaidie kuchangia gharama za kusomesha wanafunzi kwa sababu program hizo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.