*Ataka wajirekebishe ili kurudisha heshima yao
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesema wanasheria wa nchi tano za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wana kazi kubwa ya kurekebisha tabia zao na kurudisha heshima yao mbele ya jamii hasa katika masuala ya rushwa, utawala bora na demokrasia.
Waziri Pinda ametoa kauli hiyo Novemba 25, 2011 wakati akifungua Mkutano wa 16 wa Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki (East African Law Society) ulioanza jana katika hoteli ya Ngurdoto, nje kidogo ya Mji wa Arusha.
Waziri Mkuu ambaye amefungua mkutano huo wa siku tatu kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, aliwaambia wanasheria hao kwamba fani yao kwa sasa inalalamikiwa na wananchi kwa kukithiri kwa rushwa na utazoji mkubwa wa ada za uwakili na kwamba wana kazi kubwa ya kujisafisha ili kubadili muonekano wao katika jamii.
“Taarifa ya hivi karibuni ya taasisi ya Transparency International inaonesha kwamba katika nchi za Arika Mashariki, mfumo wa mahakama (judicial system) na polisi ni miongoni mwa taasisi tatu zinazoongoza kwa rushwa na uzembe unaosababisha watu kucheleweshewa haki zao,” alisema.
Alisema taasisi nyingine zilizotajwa katika taarifa hiyo ni Mamlaka ya Mapato, Uhamiaji, sekta za Ardhi, Afya na Elimu na kuongeza kwamba: “Katika idara za mahakama, ninyi wanasheria ndio waajiriwa wengi zaidi na inaposemwa kwamba maafisa wa sekta hii wanaongoza kwa rushwa ni changamoto kwetu sote ya kujaribu bila kuchoka kusafisha jina letu na kurudisha imani kwa wananchi.”
Aliwataka pia washughulikie malalamiko ya wananchi kuhusu utozaji wa ada kubwa za uwakili, mlundikano wa kesi na ucheleweshaji usio wa lazima katika kusuluhisha migogoro kama njia mojawapo wa kurudisha imani kwa wananchi wanaowategemea.
Akisisitiza kuhusu umuhimu wao katika mchakato wa kuunda Jumuiya ya Afrika Mashariki, Waziri Mkuu Pinda aliwaambia wanasheria hao kwamba wao ni sehemu ya jamii katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba hawawezi kujitenga na jambo lolote linaloiathiri jumuiya hiyo.
“Kama ni suala la kuondoa umasikini nanyi lazima linawagusa, kama ni la uchumi, mazingira au afya nanyi lazima linawagusa kwa sababu mko miongoni mwa wanajumuiya hii na maamuzi yoyote yatakayofanyika ni lazima yatawaathiri,” alisema.
Aliwataka watumie taaluma yao kuhakikisha wanatetea kuwepo kwa utawala bora na utoaji wa haki za binadamu katika nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki. “Haiwezekani leo nchi moja au mbili ziwe zinaheshimu haki za binadamu halafu nyingine zinakiuka halafu wote tuseme tuko kwenye jumuiya moja,” aliongeza.
Aidha amewataka waangalie pia uwezekano wa kuunganisha mitaala ya masomo katika nchi wanachama ili kuwa na mfumo mmoja utakaosaidia upatikanaji wa ajira kwa mujibu wa makubaliano ya soko la pamoja la ajira katika jumuiya jhiyo.
“Tuna mifumo tofauti ya elimu na mahakama kwa sababu tuliirithi kutoka kwa Waingereza, Wajerumani na Wafaransa waliotutawala… Hatuwezi kuzungumza kitu kimoja kama kila nchi itakuwa na mfumo wake. Tuangalie namna ya kuzishauri nchi zetu ili zikubaliane katika hili. Ni jukumu letu wanasheria na wala suala hili halitafanywa na wachumi, wanahisabati au wahandisi,” alisisitiza.
Akizungumzia uchumu, alisema umefika wakati wa wanasheria kupigia debe ajenda ya uchumi endelevu katika jumuiya ya afrika mashariki kwani ina wakazi zaidi ya milioni 133 na pato la Taifa la zaidi ya dola za marekani milioni 74.5. “Tuna wajibu wa kusimamia sera ambazo zitasaidia kuondoa umaskini miongoni mwa wakazi wa Afrika Mashariki,” alisema.
“Hivi sasa tumegeuzwa dampo la kuuzia bidhaa feki na Serikali zetu zinakosa mapato makubwa kutokana na watengeneza bidhaa feko. Mwaka 2008, taafifa ya Investment Climate Facility for Africa (ICF) ilionyesha kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki ilipoteza kiasi cha dola za marekani milioni 500, hiki ni kiasi kikubwa cha fedha kuacha kipotee kwani kingeweza kutumika katika ujenzi wa barabara, reli, hosptali na shule.