Pinda Awataka WanaCCM Kutupilia Mbali Uhasama wa Uchaguzi Uliopita

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amewataka wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi wasiligeuze suala la uchaguzi kuwa ni la kufa na kupona na kuwahimiza waache kuweka kinyongo baada ya uchaguzi.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Septemba 30, 2012 wakati akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa wa Katavi kwenye mkutano uliofanyika Shule ya Sekondari ya Milala wilayani Mpanda, mkoani Katavi.

“Tunapoomba nafasi hizi tusiligeuze suala hili kuwa ni la kufa na kupona. Kwani huko tunakotaka kwenda kuna nini? Ni kwa nini tunawekeana kinyongo baada ya uchaguzi wakati hii ni nafasi tu ya kuwahudumia wanaCCM wenzio?,” alihoji na kushangiliwa na wajumbe zaidi ya 1,460 kutoka wilaya za Mlele na Mpanda waliohudhuria mkutano huo.

Waziri Mkuu ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu na Kamati Kuu ya CCM aliwataka wagombea wa nafasi hizo wawe tayari kupokea matokeo kwa moyo mkunjufu na kuvunja makundi mara baada ya uchaguzi huo kukamilika. Katika uchaguzi huo, wilaya za Mpanda ziligawanywa kwa mara ya kwanza kufuatia kuundwa kwa mkoa mpya wa Katavi.

Aliwataka viongozi watakaoteuliwa wawe wanafuatilia kwa makini utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kudai taarifa za maendeleo kutoka kwa watendaji wa vijiji na kata kila baada ya miezi mitatu mitatu.

“Katibu wa Tawi una wajibu wa kumwandikia barua Mtendaji wa Kijiji (VEO) na kudai taarifa za miezi mitatu, zionyeshe mapato na matumizi… asipofanya hivyo unamwandikia barua ya kukumbusha asipotekeleza, peleka taarifa ngazi ya juu. Nasi tukipewa taarifa tutashughulikia. Tukitimua wawili watatu hivi, heshima ya kazi itarudi,” alisema huku akishangiliwa.

Katika uchaguzi uliofanyika kuanzia jana mchana hadi usiku wa manane na matokeo yake kupatikana saa 9 alfajiri, Bw. Philip Kalyalya aliibuka kidedea kwenye nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mlele kwa kupata kura 500 na kuwabwaga wapinzani wake Bw. Jacob Mambosasa (kura 111) na Bw. Joseph Msabaha (100).

Katika nafasi za ujumbe wa NEC Taifa, Bw. Thomas Kampala aliibuka mshindi kwa kura 436 na kumbwaga mpinzani wake Jacob Msyete aliyepata kura 250. Nafasi za wajumbe watano wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa zilinyakuliwa na Bi. Winfrida Katabi (420), Nyasongo Serengeti (357), Emmanuel Pondamali (305), Pascal Sanane (262) na Augustino Mbalamwezi (237).

Kwa upande wa wilaya ya Mpanda, Bw. Beda Katani aliibuka mshindi kwa kupata kura 472 na kumshinda Bi. Fulgensia Kapama aliyepata kura 208. Kwenye ujumbe wa NEC Taifa, Bw. Suleiman Kakoso aliibuka mshindi kwa kupata kura 352 na kuwashinda Bw. Pius Bizumale (kura 235) na Bw. Gabriel Mnyele (kura 85). Bw. Kakoso ni Mbunge wa jimbo la Mpanda Vijijini.

Wajumbe watano walioshinda nafasi za Mkutano Mkuu wa CCM Taifa na kura zao kwenye mabano ni Bw. Sebastian Kapufi (512), Bw. William Mbogo (424), Bw. Michael Kapata (275), Bw. Ramadhan Kala (242) na Bw. Yasini Katampa (206). Wilaya zote mbili pia zilifanya uchaguzi wa wajumbe wa CCM Mkoa, Halmashauri ya CCM Wilaya kupitia makundi ya Wazazi, UVCCM na UWT.