Pinda awalainisha madaktari, warejea kazini

Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiwaaga madaktari jana mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo nao yaliozaa matunda na kumaliza mgomo.

Na Mwandishi Wetu

MIKUTANO iliyofanyika mfululizo tangu juzu kati ya makundi mbalimbali ya madaktari pamoja na Waziri Mkuu Mizengo Pinda imezaa matunda baada ya Serikali kufanikiwa kuwarejesha madaktari kazini.

Jana Serikali imekubaliana na madaktari warejee kazini huku ikianza kuchukua hatua kwa hoja zao, ambapo tayari Serikali imemsimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Deo Mtasiwa.

Pinda amefikia hatua hiyo jana na taarifa zinasema viongozi hao wamesimamishwa kupisha uchunguzi katika ofisi zao juu ya mgogoro uliyokuwepo kati ya madaktari hadi kusababisha mgomo.

Hii ni hatua ya kwanza ya Serikali kuanza kuyafanyia kazi madai kadhaa ya madaktari yaliyowasilishwa Serikalini, huku wakikubaliana na madaktari kupewa mwenzi mmoja kuangalia namna ya kutatua hoja nyingine ambazo zitaweza kufanyiwa kazi na Serikali.

Madaktari wameridhia kurejea kazini huku Serikali ikijipanga kufanyia kazi baadhi ya madai ambayo yataweza kutatuliwa ndani ya mwezi mmoja. Kuhusua suala la kujiuzulu kwa waziri wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Naibu wake Pinda amemwachia Rais Jakaya Kikwete kwani ndiye aliyewateua na anauwezo wa kuangalia utendaji wao.

Taarifa ambazo mtandao huu umezipata ni kwamba Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Ananilea Nkya pamoja na Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Helen Bikijo-Simba wamekamatwa na polisi jana kwa mahojiano, kutokana na maandamano waliyoyafanya juzi Daraja Salenda kushinikiza Serikali kuchukua hatua mgomo wa madaktari. Taarifa zaidi zitakujia hapo baadaye.