*Asema wasiojua pato la wanaowaongoza hawafai
Na Mwandishi Maalumu
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema kuwa wakuu wa mikoa, wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri wasiojua kipato halisi cha wananchi wao hawafai kuwa viongozi katika maeneo waliyopo. Amesema kuwa kiongozi mzuri ni lazima afahamu viashiria mbalimbali kama hali za wananchi na maendeleo yao ili atambue namna ya kuwasaidia zaidi kujikwamua na hali ngumu za maisha.
Waziri Mkuu aliyasema hayo Ijumaa, Septemba 16, 2011 mara baada ya kupokea taarifa ya Mkoa wa Mara ambako amewasili na leo anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi ya siku saba.
“RC, DC, DED na viongozi wengine ambao wanashindwa hata kujua pato la mwananchi ambalo ndilo linawawezesha kupima hata ubora wa maisha yao, basi hawafai hata kidogo… jifunzeni kutathimini hali za wananchi wenu kwa kuwa itawawezesha kuwasaidia zaidi,” alisema.
Alisema kuwa mkoa huo ni wa 14 kati ya mikoa 21 ambapo wastani wa pato la mwananchi wa Mara kwa mwaka ni sh. 642,000/- ambazo zikigawanywa kwa mwezi na hadi siku inaonekana kipato hicho ni kidogo ikilinganishwa na mikoa mingine inayoizunguka Mara.
“Wenzenu hapo Arusha kipato cha mwananchi kwa mwaka ni sh. 950,000/-; Mwanza ni sh. 830,000/-; hivyo lazima mketi na kutafakari ni kwa nini mnakuwa nyuma ya hao majirani zenu huku mkiwa na fursa nyingi kuwazidi hao. Fanyeni kazi ya ziada kuhakikisha mnatumia vema rasilimali zilizopo ili mpige hatua inayostahili,” alisema.
Waziri Mkuu alikwenda mbali na kusema kuwa mkoa huo haukuwa na sababu hata ya kuomba msaada wa chakula Serikalini kwa kuwa takwimu zinaonesha walizalisha zaidi lakini hawakuwa na nidhamu katika matumizi ya chakula hicho.
“Si sahihi hata kidogo kujikuta mkiomba chakula Serikalini, changamoto hii ifanyieni kazi kwa kuhakikisha chakula kinachopatikana kinatosheleza kwa kula na kinachobaki kinaweza kufanyiwa mambo mengine lakini kwa tahadhari kubwa,” alionya.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Wakuu wa Mikoa minne na wakuu wa wilaya mpya 19 watateuliwa haraka iwezekanavyo mara baada ya kukamilika kwa mchakato wa maoni ya kuunda mikoa mipya na wilaya mpya unaotarajiwa kukamilika Oktoba 5, mwaka huu.
“Najua mmesikia haya mabadiliko ya uongozi yaliyofanywa na Rais katika nafasi za Wakuu wa Mikoa na kwa hapa Mara mna mkuu mpya, Bw. John Tupa ambaye naamini atawasaidia sana kutokana na uzoefu wake alionao hivyo mpeni ushirikiano wa kutosha kwa upande wa Serikali na vyama,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema kuwa mara baada ya kukamilika kwa mchakato wa maoni ya mikoa na wilaya zilizotangazwa kwenye gazeti la Serikali, Rais atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufanya uteuzi wa wakuu wa mikoa hiyo minne na wilaya mpya 19.
Kwa upande wa wilaya ambazo wakuu wake wamepandishwa vyeo na kuwa Wakuu wa Mikoa, Waziri Mkuu aliwataka wananchi wa wilaya hizo kuwa wavumilivu wakati mchakato wa kujazwa nafasi hizo ukifanyika. Rais Jakaya Kikwete aliwateua Wakuu hao wa mikoa wapya ambao waliapishwa Septemba 16, 2011 Ikulu, jijini Dar es Salaam na kati ya wateuliwa hao, jumla ya waliokuwa Wakuu wa Wilaya 11 walipandishwa vyeo na kuwa Wakuu wa Mikoa.