Na Joachim Mushi
WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda amewataka wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha wanasimamina vizuri suala la kilimo ili kuleta mapinduzi kama ilivyo kwa sera za Serikali.
Pinda ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akifunga rasmi Maonesho ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyokuwa yakifanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere.
Waziri Mkuu Pinda amesema viongozi hao hawana budi kusimamia ipasavyo sekta ya kilimo ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Nne ambayo imekuwa ikichukua hatua anuai kuboresha kilimo ambacho ni uti wa mgogo wa taifa.
Aidha Pinda amesema nchi imeadhimisha miaka 50 ya Uhuru ikiwa imepiga hatua kubwa ya maendeleo ya kiuchumi. Amesema miaka ya 1960 ukuaji wa uchumi ulikuwa wa asilimia 4, ilhali sasa hadi mwaka jana ukuaji umepanda na kufikia asilimia 7, ambapo Tanzania ni tika kundi la nchi 20 zinazokuwa kwa kasi kiuchumi.
Hata hivyo amebainisha kuwa changamoto kubwa inayolikabili Taifa kwa wakati huu ni namna ya kuendeleza mafanikio yaliopatikana kiuchumi na kuhakikisha yanaonekana wazi kwa hali za maisha kwa wananchi.
Maonesho hayo yaliyokuwa yakielezea zaidi mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kwa kipindi chote tangu Taifa lipate Uhuru, yameshirikisha Wizara zote, Halmashauri zote nchini pamoja na washiriki 18 kutoka mataifa anuai nje ya Tanzania.