Pinda ataka halmashauri zitenge maeneo ya Benki ya Ardhi

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amezitaka Halmashauri za Wilaya nchini kutenga maeneo maalum kwa ajili ya uwekezaji ili baadaye yatumike kama land bank (akiba ya ardhi) kwa urahisi.

Amesema watendaji wa Halmashauri wakishatenga maeneo hayo, hawana budi kuwasiliana na Mamlaka ya Kuendeleza Maeneo Huru ya Uwekezaji (EPZA) ili wanapojitokeza wawekezaji maeneo hayo yawe yamekidhi vigezo vinavyohitajika.

Ametoa kauli hiyo Oktoba 17, 2011, wakati akifunga mkutano wa siku moja wa uwekezaji wa Kanda ya Uwekezaji ya Ziwa Tanganyika (Lake Tanganyika Investors’ Forum) uliofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda, mkoani Rukwa.

“Katika mada ya EPZA na SEZ, tulionyeshwa suala moja muhimu lililohusu kutenga maeneo… katika hili ni Kigoma peke yao ambao wamefanya vizuri. Wameainisha maeneo ya viwanda, kilimo na makazi. Tujipange ili EPZA wakitaka maeneo wakute yako tayari,” alisema.

Alisema suala jingine linalohitaji msukumo ni utoaji elimu ya kutosha kwa wanachi ili kuondoa upotoshaji kuhusu uwekezaji unaofanyika ama kwa makusudi ama kwa kutokujua.

“Wananchi waelimishwe kwamba kuna makundi mbalimbali ya wawekezaji na kama alivyosema Mhe. Rais Kikwete, katika nafasi yao, wakulima wadogo ni wawekezaji, wapo wajasiriamali wadogo na wa kati na pia wako wakulima wakubwa au wawekezaji wakubwa.”

Alisema ushirikishwaji wa jamii ni muhimu na kwamba viongozi hawana budi kushuka hadi katika ngazi ya vijiji ili kuwaelewesha wananchi uhusiano uliopo baina ya uwekezaji na uwepo wa maendeleo. “Suala la kushirikisha wananchi ni la msingi, tushuke katika vijiji na kuwaelimisha …”, alisema.

Alisema akiwa katika ziara ya mkoa wa Mara mwishoni mwa mwezi uliopita, aliwashauri wawasiliane na mikoa jirani ya kanda ya ziwa ili waangalie uwezekano wa kuunganisha nguvu zao katika suala la uwekezaji kwani wana fursa zinazoshabihiana kutokana na sababu za kijiografia.

“Nimemweleza Mhe. Rais kuhusu wazo hili naye akalikubali na kunipa kazi nyingine ya kuangalia uwezekano wa kuunganisha mikoa ya Tanga, Morogoro na Pwani ili nayo ijumuike na kuunganisha nguvu katika kutafuta fursa za uwekezaji walizonazo, ikiwezekana nao pia wafanye mkutano wa pamoja.

Waziri Mkuu aliiagiza sekretarieti iliyosimamia maandalizi ya mkutano huo, iweke muda maalum katika maazimio yaliyotolewa na kuandaa kijitabu kitakachokuwa na maelezo ya mkutano huo ili kiwe dira ya kuwasukuma kufikia ndoto waliyoianza ya kuwa na ukanda wa ziwa Tanganyika wenye maendeleo ya kutosha.

Mapema, wakichangia mada zilizotolewa katika mkutano, washiriki wengi walisema mbali ya msukumo uliopo kuhusu uwekezaji, kuna haja kubwa ya kuhakikisha kuwa nishati ya uhakika inakuwepo ili kuvutia viwanda vya usindikaji mazao ambavyo vitaleta ajira na kupunguza umaskini miongoni mwa wananchi.

Washiriki wengine wa mkutano huo ambao kaulimbiu yake ilikuwa “Kuibua Fursa za Uwekezaji katika Kanda ya Ziwa Tanganyika” (Unleashing Potentials for Lake Tanganyika Zone) walitaja vikwazo wanavyokumbana navyo wakati wakitafuta maeneo ya uwekezaji na kusisitiza kuwa urasimu upunguzwe ili kuharakisha maendeleo katika kanda hiyo.

Mkutano huo ambao ulifunguliwa jana na Rais Jakaya Kikwete ulikuwa na lengo la kuinua fursa za uwekezaji katika Kanda ya Uwekezaji ya Ziwa Tanganyika ambayo inaihusisha mikoa ya Rukwa, Kigoma na mkoa mpya-tarajiwa wa Katavi ambayo yote kwa pamoja imejaaliwa maliasili nyingi zikiwemo madini, vivutio vya utalii, ardhi nzuri ya kilimo na maeneo ya uvuvi.