WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema uongezaji virutubisho kwenye vyakula umeibua mguso mpya na kuleta mlipuko baina ya sekta binafsi na sekta za umma (PPP) ambazo zinasimamia masuala ya afya kwa kiwango kikubwa.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema kazi kubwa zaidi inabidi ifanyike ili elimu ya kutosha iweze kufikishwa kwa mabilioni ya watu ambao milo yao ya kila siku haina virutubisho vya kutosha.
Ametoa kauli hiyo jana usiku (Jumatano, Septemba 9, 2015) wakati akizungumza na washiriki zaidi ya 400 kutoka nchi 30 wanaohudhuria mkutano wa kwanza wa kimataifa wa urutubishaji vyakula ulioanza jana jijini Arusha. Mkutano huo utamalizika kesho, Septemba 11, 2015.
“Bila kuwa na sera zinazoeleweka na jamii, bila kuwekeza zaidi na bila kuwa na timu ya wataalamu waliobobea kwenye masuala la chakula, tuko hatarini kupoteza kasi tuliyoanza nayo na tunaweza tusifanikiwe kutimiza malengo tuliyotarajia,” alionya Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu ambaye alifungua mkutano huo kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, alisema urutubishaji wa vyakula unaohimizwa ni uongezaji wa madini na vitamini kwenye vyakula vinavyosindikwa viwe vya mafuta au nafaka ili kupambana na udumavu na utapiamlo. Alisema hivi sasa virutubisho vinavyoongezwa kwenye vyakula ni pamoja na madini ya chuma, zinc, vitamini A na vitamini B12.
“Uongezaji wa virutubisho unaendana na kampeni ya siku 1,000 za mwanzo wa maisha ya mtoto (1,000 days of a child’s life) ambayo inaendeshwa na Serikali yetu kwa kuzingatia kuwa faida zake zinagusa ukuaji na afya ya mtoto, ukuaji wa ubongo wa mtoto, ujenzi wa kinga imara za mwili, uelewa mkubwa unaomwezesha mtoto kufanya vizuri masomoni na uhakika wa maisha marefu ambao unachangia ukuaji wa uchumi na pato la Taifa,” alisema.
Kuhusu juhudi za Serikali, Waziri Mkuu alisema Serikali kupitia Mamlaka ya Serikali za Mitaa imelenga kupanua huduma za urutubishaji wa vyakula vijijini ambako asilimia 70 ya Watanzania wanaishi. “Mifumo imewekwa ili kusaidia wenye viwanda vya kusindika nafaka na mafuta waweze kuongeza virutubishi hivyo,” alisema.
Alisema Tanzania ilianza kampeni za kuongeza virutubisho kama vile madini joto (iodine) kwenye chumvi tangu miaka ya 90 na matokeo yake hivi sasa hakuna wagonjwa wa goitre kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Hivi sasa kila kaya inatumia chumvi yenye madinijoto na asilimia zaidi ya 80 ya kaya zinatumia chumvi ya aina hii. Matokeo yake ni kupungua kwa ugonjwa wa goitre na kufikia chini ya asilimia tano kwa watoto wenye umri kati ya miaka 6-12 ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kwenye miaka ya 1980,” alifafanua.
Kwa upande wake, Balozi wa Umoja wa Afrika (AU) wa Masuala ya Kupambana na Njaa, Mfalme Letsie III wa Lesotho alisema suala la kurutubisha vyakula lisiachwe kuwa la Serikali peke yake bali linahitaji nguvu ya pamoja kutoka kwa wadau mbalimbali na hata ikibidi Serikali zote za Bara la Afrika.
“Vyanzo vya upungufu wa virutubisho na utapiamlo na vingi na vina njia mbalimbali za kukabiliana nazo. Lakini hapa nataka nisisitize kwamba, tunahitaji utashi wa kisiasa kutoka kwa wakuu wa nchi zote duniani na siyo kwa bara la Afrika peke yake ili suala hili liweze kufanikiwa,” alisema.
“Nikiwa Balozi wa AU wa kupambana na njaa, ninazitaka nchi zote na Serikali zilizoko madarakani ziweke sheria mahsusi au sera za kitaifa ambazo zitaweka bayana suala la urutubishaji wa vyakula kama njia ya kupambana na njaa na pia kumaliza kabisa tatizo la upungufu wa virutubisho vya kutosha kwenye milo ya kila siku ya watu wetu,” alisema huku akishangiliwa.
Naye Naibu Waziri wa Afya, Dk. Kebwe S. Kebwe alisema Serikali imelenga kuajiri maafisa lishe kwenye Halmashauri za Wilaya 157 ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa viinilishe kwenye vyakula.
Alisema kati ya mwaka 2010 na 2013 Serikali imeongeza kiasi cha fedha kutoka sh. bilioni 19/- hadi sh. bilioni 33/- ili zisaidie kusimamia masuala ya lishe na urutubishaji wa vyakula.
Mapema, akitoa taarifa kuhusu Mkutano huo wa Kwanza wa Kimataifa, Mkurugenzi Mtendaji wa Global Alliance for Improved Nutrition (GAIN), Dk. Marc Van Ameringen alisema mkutano huo unawajumuisha watendaji kutoka serikalini, taasisi binafsi, vyuo vikuu na taasisi za utafiti ili kwa pamoja waje na suluhisho la kudumu juu ya urutubishaji vya vyakula kama njia ya kupambana na njaa na udumavu.
Alisema wana maeneo matano ambayo wameyalenga yakiwemo uboreshaji wa sheria; utoaji wa elimu zaidi na ushawishi kwa jamii; haja ya kupata uwekezaji zaidi kwenye eneo hilo; haja ya kupata msukumo kutoka Serikali za nchi mbalimbali na kuhakikisha kuwa urutubishaji wa vyakula unaingizwa kwenye mikakati ya kitaifa.