Pinda asikitishwa na Tanzania Daima

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda

Na Mwandishi Maalumu

OFISI ya Waziri Mkuu imesikitishwa na habari iliyochapishwa na gazeti la Tanzania Daima toleo namba 2610 la Januari 26, 2012, kwenye ukurasa wake wa kwanza yenye kichwa cha habari:

“Dk. Mwakyembe aipasua Serikali”
*Pinda amtaka azungumzie hali yake *Aunga mkono posho za Wabunge kupanda *Adai wanaosaka Urais hawana akili nzuri

KWENYE habari hiyo iliyopewa uzito wa juu kwenye ukurasa wa kwanza na kuendelea ukurasa wa pili kuna taarifa inayosema kwamba Waziri Mkuu amedai kuwa wanaowania kugombea urais mwaka 2015 hawana akili nzuri.

Gazeti la Tanzania Daima liliandika: “Mimi nimeshasema sitagombea ubunge, wala urais mwaka 2015, lakini mtu anayehaha kuutaka urais hawezi kuwa na akili nzuri hasa kama kweli anajua Ikulu anakwenda kufanya nini”.

Habari hii haina ukweli wowote kwani Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema wanaoutaka urais hawajui ugumu wa kazi hiyo. Alichosema Waziri Mkuu ni hiki: “Wanaotaka urais hawajui urais ni kitu gani, waendelee nao, lakini mimi naona hapa (Ikulu) ni kazi ngumu tu kwa sababu hulali… napajua hapa, nimetumia sehemu kubwa ya maisha yangu ya utumishi nikiwa Ikulu.

“Haiwezekani mtu ukautaka urais, isipokuwa kama unachofuata State House ni mazingira yake ama kujinufaisha na siyo kubebeshwa mzigo wa kusaidia Watanzania…”

Katika habari hiyo, mwandishi wa Tanzania Daima alimnukuu Waziri Mkuu akisema kwamba alikutana na John Malecela na kumwambia kwamba anajiona ameutua mzigo mzito. Alichoandika mwandishi huyo:

“Wakati Mwalimu Julius Nyerere anang’atuka siku moja tulikwenda nyumbani kwake Msasani. Tukiwa tumekaa naye, alikuwa anamtania John Malecela, akamwambia: ‘John, hapa nilipo naona kama kuna kitu kikubwa kimetoka mwilini mwangu, najiona mwepesi sana.”

Katika mkutano wake na Wahariri wa vyombo vya habari, Jumatano, (Januari 25, 2012) hakumtaja kabisa, John Malecela bali alimtaja Mama Joan Wickens ambaye alikuwa Msaidizi wa Mwalimu Nyerere (Personal Assistant) wakati huo.

Alichosema Waziri Mkuu: “Labda niwape mfano, siku Rais Nyerere anang’atuka, alipotoka Uwanja wa Taifa kuagwa rasmi, alifika nyumbani akapanda juu, alipoteremka akatukuta watu watatu, mimi, Mzee Batao na Mama Joan Wickens. Mimi nilikuwa kijana wakati huo (1985), natumwa tu hamisha faili peleka hili pale…”

“Mwalimu alimwambia msaidizi wake, Joan Wickens (marehemu), kwamba anajisikia faraja kama mtu aliyeondokewa na kitu fulani mwilini. Alionekana kama katua mzigo mzito uliokuwa unamwelemea…”

Ofisi ya Waziri Mkuu inasikitishwa na taarifa hizo za uchochezi na upotoshaji. Ni vema mwandishi angeuliza kupata ufafanuzi na kupata usahihi wa majina yaliyotumiwa kabla ya kuchapisha habari hizo. Kama gazeti, Tanzania Daima lilipaswa lijiridhishe na usahihi wa habari zake kabla ya kuzichapisha kama inavyoelekeza misingi mikuu ya uandishi wa habari na weledi wa kazi hiyo.

Uandishi wa habari za uongo hauna maana, unaleta hofu na unaweza kuchochea hisia ambazo hazipo bila sababu za msingi miongoni mwa wananchi. Na hiyo siyo kazi ya uandishi wa habari.