Pinda asema Serikali itaendelea kuboresha sekta ya umma, sheria na fedha

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda

Na Mwandishi Maalumu

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda amesema Serikali itaendelea kufanya maboresho kwenye sekta za umma, fedha, sheria za Serikali za Mitaa ili kuondoa urasimu katika mifumo ya kiutawala.

Pinda ametoa kauli hiyo leo mchana Januari 26, 2012 akifungua Mkutano wa Tatu wa kila mwaka wa majadiliano ya kisera baina ya Serikali na Wadau wa Maendeleo kwenye Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.

Ametumia fursa hiyo kuwaomba wadau wa maendeleo nchini wanaohudhuria mkutano wa siku mbili ambao umeanza leo, kuendelea kuisaidia Serikali katika kufadhili mpango wa maboresho kwa vile utasaidia kupunguza vikwazo vinavyochangia kuchelewa kwa baadhi ya maamuzi.

Waziri Mkuu aliwaomba Watanzania wote kwa pamoja kuisaidia Serikali kusukuma mele ajenda ya maendeleo ambayo itaifanya Tanzania kuwa Taifa la kisasa katika karne ya 21.

“Ni vizuri kama watu mnaweza kukaa pamoja, kujadili matatizo mliyonayo, kutafuta njia za kuyatatua na kufanya maamuzi haraka na kwa njaia sahihi. Tuache utamaduni wa kulalamika na badala yale tuwe wachapakazi wenye nia ya kuona matokea ya haraka,” alisema.

“Changamoto kubwa tuliyonayo, siyo kwamba hatuelewi matatizo yanayotukabili au nini kinapaswa kifanyike ili tujikwamue kutoka kwenye umaskini, bali ni njia gani tutumie ili kuondokana na tatizo hilo,” alisisitiza.

Alisema wakati umefika sasa wa kuamua kufanya maamuzi sahihi na ya pamoja na wakati huo si mwingine bali ni sasa. “Tufanye maamuzi sasa na lazima tuanze sasa,” alisema.

Mapema, akizungumza kwa niaba ya washirika wa maendeleo, Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa hapa nchini ambaye pia ni Mwenyekiti Mweza wa Kundi la Wahisani (Development Partners Group Co-Chair), Alberic Kacou alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Tanzania imeonyesha mafanikio ya kutosha katika nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Alisema licha ya mafanikio hayo, bado Tanzania inakabiliwa na changamoto ya kupunguza umaskini kwa wananchi wake kwa mujibu wa kiashiria cha kupima maendeleo ya wananchi katika nchi mbalimbali (Human Development Index – HDI).

“Kwa mujibu wa kiashiria cha kupima maendeleo ya wananchi katika nchi mbalimbali, asilimia 65 ya Watanzania bado wanaishi katika umaskini kwa kukosa elimu, huduma za afya, maji safi na salama, umeme, nishati ya kupikia na mali,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Bi. Esther Mkwizu alisema Serikali haina budi kuwekeza kwa nguvu zaidi kwenye rasilimali watu kama njia mojawapo ya kukuza uchumi lakini zaidi kujenga Taifa lenye watu weledi.

Alisema Uswisi ni nchi ambayo ilipoteza nguvukazi kubwa wakati wa vita ya dunia, lakini sasa hivi ni mojawapo ya tajiri duniani kwa sababu ilitumia rasilmali watu kama mtaji wa kukuza uchumi wake.

“Ni nchi ambayo haina bandari wala kivutio chochote cha maliasili kama tulivyonavyo sisi, lakini ni miongoni mwa nchi tajiri kwa sababu iliwekeza katika wananchi na sasa inawatumia katika kazi mbalimbali ulimwenguni,” aliongeza.