WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amerejea jijini Dar es Salaam akitokea Dodoma kwa ajili ya kushughulikia mgomo wa madaktari ambao unaendelea maeneo mbalimbali ya nchi, na kuupatia.
Taarifa zinasema Waziri Pinda baada ya kufika amekutana na uongozi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili pamoja na madaktari bingwa kutoka sekta ya umma, binafsi pamoja na wale wastaafu.
Kesho saa tatu asubuhi Waziri Pinda atakutana na madaktari bingwa, madaktari waliosajiliwa na madaktari ambao wapo kwenye mafunzo ya vitendo (interns) na baada ya hapo saa nne atakutana na wafanyakazi wa Hospitali ya Muhimbili, MOI, OCEAN ROAD na wawakilishi kutoka hospitali za mkoa wa Dar es Salaam kwenye Ukumbi wa CPL, Muhimbili.
Matarajio ya Serikali ni kwamba mazungumzo hayo yataweza kumaliza mgogoro huu na madaktari wote kurejea kazini na hivyo kurejesha huduma za matibabu katika hali ya kawaida kwa wananchi wa Tanzania. Hivyo Serikali inawaomba wote wanaohusika wafike katika mikutano hiyo bila ya kukosa. Imetolewa na ofisi ya waziri mkuu.