WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amepiga marufuku ukarabati wa maabara za shule za sekondari na kusisitiza kwamba ni lazima zijengwe mpya kama ambavyo Serikali ilielekeza. Ametoa agizo hilo leo Februari 21, 2015 wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa kata ya Ilula, mara baada ya kukagua ukarabati wa maabara za sayansi kwenye shule ya sekondari Ilula, wilayani Kilolo, mkoani Iringa.
“Mmefanya ukarabati kwenye jengo lililojengwa zaidi ya miaka 20 iliyopita. Kuna chumba nimekuta ni kidogo mno sababu hakiendani na specifications za sasa…chumba kimoja kimepasuka ukuta, hapana! RC kama kuna nyingine ya aina hii kazi isiendelee,” alisema.
“Huu ukarabati mliofanya ni kinyume na maelekezo ya Serikali ya kutaka zijengwe maabara mpya. Tulisema zijengwe maabara mpya ili ziweze kudumu kwa miaka mingi kidogo. Kuna chumba ceiling board iko chini kwa sababu ujenzi ni wa zamani. Ujenzi wa sasa mapaa yako juu zaidi ili kuruhusu hewa ya kutosha,” aliongeza.
“Ningeweza kusema vunjavunja lakini haitakuwa haki kwa sababu kuna fedha za watu zimetumika… kwa sasa yatatuhifadhi kwa muda kidogo, lakini haya majengo hayatadumu hata kidogo,” alisema.
Waziri Mkuu pia alikataa kuahidi mchango aliiombwa achangie na kuwaeleza kwamba atakuwa tayari kuchangia ujenzi wa jengo jipya na siyo ukarabati kwani huo utakuwa ni upotevu wa fedha. Majengo aliyoonyeshwa Waziri Mkuu Pinda yalijengwa mwaka 1995 na yalikuwa yakitumika kama maabara kwenye sekondari hiyo.
Alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bibi Amina Masenza asimamie watu wake ili ujenzi wa maabara uweze kukamilika kwa muda uliopangwa. Mkoa huo unahitaji mabaara 72 na zilizokamilika ni maabara tano tu huku nyingine 53 zikiwa kwenye hatua mbalimbali za ujenzi na 13 bado ziko kwenye msingi na moja iko kwenye linta.
Mapema, akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mtendaji wa Kata ya Ilula, Bw. Titus Katemo alisema shule ya sekondari Ilula ilijenga maabara zake mwaka 1995 kwa nguvu za wananchi na kwamba zilikuwa zikitumika toka kipindi chote hicho.
Alisema ili kuendana na matakwa ya Wilaya, ukarabati wa vyumba vitatu ulianza Novemba 15, mwaka jana kutokana na vyumba hivyo kutumiwa na watahiniwa wa kidato cha nne wa mwaka 2014 kwenye mitihani ya vitendo.
“Makisio ya gharama za ukarabati wa vyumba vitatu yalikuwa ni sh. 38,294,775.00 na tunatarajia ukarabati utakamilika ifikapo tarehe 30 Machi 2015,” alisema na kumuomba Waziri Mkuu awasaidie awaunge mkono kwa mchango kwani kasi ya wananchi kuchangia imekuwa ndogo.
Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake wilayani Kilolo na mchana huu anaenda kukagua mradi wa umwagiliaji wa Nyanzwa na pia atazungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara.