Pinda akemea viongozi wasiojali shida za Watanzania

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglican nchini, Valentino Mkokiwa (katikati) katika Ibada ya kumweka wakfu Askofu Maimbo William Mdolwa (kulia) wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Tanga iliyofanyia kweye viwanja vya Chuo cha Ualimui cha Korogwe, Septemba 4, 2011. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

*Askofu Mtemelelwa atema cheche

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amekemea viongozi wasiojali na kushughulikia kero za watu na umaskini unaowazunguka watu wanaowaongoza na akawataka viongozi wa madhehebu ya dini waisaidie Serikali katika kupambana na hali hiyo.

Ametoa kauli hiyo jana Septemba 4, 2011 akitoa salamu za Serikali kwenye ibada ya kumuweka wakfu Askofu Mteule, Maimbo Mndolwa wa Kanisa la Anglikana Tanzania iliyofanyika kwenye kwenye Viwanja vya Chuo cha Ualimu Korogwe jirani na Kanisa la Mt. Mikaeli na Malaika Wote mkoani Tanga.

Alisema viongozi wote wakiwemo Maaskofu, Wachungaji, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya kila mmoja hana budi kuumia kutokana na matatizo yanayowakabili Watanzania ili kurudisha imani ya wananchi.

“Tuna kazi kubwa ya kuwatoa Watanzania katika lindi la umaskini…kila mmoja adhamirie kujiondoa katika ubinafsi, mmezungumza suala la upendo. Katika hali ya kawaida, mtu huwezi kukosa upendo kwa jirani halafu ukadai kuwa wewe ni muadilifu…,” alisema.

Alisema kila mmoja anapaswa kuhakikisha anasimamia jambo hilo kwa sababu ni la Watanzania wote. “Tukiwa waadilifu ndipo nchi itakwenda kwa amani,” alisisitiza.
“Mtu akishapata nafasi ya uongozi ni rahisi sana kushawishika kuitumia vibaya nafasi aliyonayo kwa kujilimbikizia mali… kama hakuna uadilifu iko siku tutachapana viboko. Ni lazima dini zote tuendelee kusema lugha moja ya kusisitiza uadilifu,” alisema.

Alisema viongozi wa dini wanasikilizwa zaidi na jamii hivyo wana nafasi kubwa ya kutoa ushawishi ili waumini wao wasijihusishe na vitendo viovu na kwamba wana uwezo mkubwa wa kuisaidia serikali kupambana na mmomonyoko wa maadili katika jamii.

“Ninawaomba tushirikiane kutokomeza maovu yanayoiandamana jamii, ninawaomba mtumie nafasi yenu katika jamii hasa ile ya kuponya kiroho kuwarudisha Watanzania wengi waliopotoka katika maadili mema…,” alisema. Aliwaomba viongozi wa kanisa watumie fursa ya ufugaji nyuki kwa kuhimiza kila familia iwe na mizinga walau mitatu hadi mitano kwani ni njia ya uhakika ya kuleta kipato kwa wananchi wa kawaida.

“Kila mzinga mmoja unaweza kumpatia mkulima au mfugaji lita 10 katika miezi mitatu na kila lita moja ni sh. 10,000/-. Kwa hiyo ni sh. 100,000/- kwa kila mzinga. Tuhimize waumini wetu wafuge nyuki sababu Tanga mna uoto mzuri wa asili na maji yapo. Kwa njia hii tutawawezesha wananchi kumudu kulipa ada za watoto…,” alisema.

Mapema, akitoa mahubiri katika ibada hiyo, Askofu Mstaafu Donald Mtetemelwa alisema anatamani viongozi wote wangekuwa waadilifu na zaidi ya yote watambue ni kwa nini Mungu aliwaita kwenye nafasi hizo za uongozi na jambo gani wanapaswa kufanya kwa ajili ya watu wao.

“Kiu ya watu wengi leo hii ni kupata mtu wa kuwaongoza mwenye utu, upole na anayewajali. Viongozi wengi wa sasa wanapata tamaa ya mali kwa sababu hawana kitu kipya ndani yao cha kuwasukuma wawe waadilifu.”

Alisema kiongozi wa watu ni lazima awe ameguswa na hali mbaya za watu anaowaongoza. “Ukiwa na mzigo na shida za watu wako, utaona uchungu na taabu zao, utataka watoke katika hali hiyo na utamuomba Mungu akusaidie kutatua shida zao,” alisema.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda


“Viongozi wengi wanafanya uhalifu kweupe sababu ndani yao hamna Mungu, wanaenda kwa asili yao (akimaanisha mazoea ya kujilimbikiza mali) bila kujali uzuri wa kitu walichonacho,” alisema huku akishangiliwa. Alimtaka Askofu Mndolwa ambaye amewekwa wakfu leo ajishushe na kuwa karibu na watu anaowaongoza ili aweze kujua matatizo yanayowakabili waumini wake. “Nenda waliko watu, ukaonekane waliko wenye dhambi…ushuke kwao ili uishi nao siyo kujifungua ofisini,” alisisitiza.

Askofu Mndolwa ambaye anakuwa Askofu wa Pili wa Dayosisi ya Tanga, alizaliwa Novemba 24, 1969 katika kijiji cha Baamoyo, Ambanguli wilayani Korogwe, Tanga. Kabla ya hapo, alikuwa Mkuu wa Chuo wa Mt. Marko kuanzia Agosti 2008 hadi Januari 2010 alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Shule yaTheolojia ya Chuo Kikuu cha St. John kituo cha Dar es Salaam. Bado alikuwa anafanya utafiti wa digrii yake ya Uzamivu katika Chuo Kikuu cha KwaZulu Natal cha Afrika Kusini. Ameoa na ana watoto wawili.

Ibada hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Nchi, (OWM-TAMISEMI), Bw. George Mkuchika, wabunge wa mkoa wa Tanga, wakuu wa wilaya wanane, maaskofu 16 akiwemo Askofu Mstaafu John Ramadhani na Askofu Mstaafu wa Dayosisi ya Tanga, Dk. Philip Baji. Pia walikuwepo mapadri kutoka Dayosisi 25 za Kanisa la Anglikana Tanzania.